Mwandishi Wetu, Zanzibar
BEI za bidhaa za vyakula Zanzibar na vitongoji vyake hazijapanda kama ilivyodaiwa na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Jussa Ismail Ladhu.
Akizungumza kwenye soko la Mwanakwerekwe mara baada ya ziara ya kukagua bei za bidhaa za vyakula sokoni hapo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Muhsin Ussi ambaye aliambatana na Katibu Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, hakuna bidhaa zilizopanda.
Muhsin alisema, licha ya wao kufika sokoni hapo kwa ajili ya kununua mahitaji, lakini pia wamefuatilia kujua ukweli na kubaini hakuna chakula kilichopanda bei.
Muhsin alisema, hivi karibuni Jussa aliviambia vyombo vya habari kuwa bidhaa katika masoko ya Zanzibar bei zimepanda kutokana na Serikali ya Mapinduzi (SMZ), kuzichelewesha meli bandarini kushusha mizigo zikiwemo bidhaa za vyakula hivyo kusababisha kadhia hiyo.
“Tumejionea bidhaa zipo za kutosha na watu wapo katika pilika pilika za manunuzi,” alisema na kuongeza kuwa, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesimamia suala hilo kuhakikisha bidhaa zinapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu na elekezi ili kila mmoja atimize Ibada ya Ramadhan kwa amani na utulivu.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza sokoni hapo walisema, wana bidhaa za kutosha na bei ni rafiki, huku wateja nao wakisisitiza kuhusu suala la bei na upatikanaji wa bidhaa.
“Bidhaa zipo za kutosha, zimeongezeka sana na hata bei ni ya kawaida sana,” alisema mmoja kati ya wateja sokoni hapo, Salim Said Suleiman.
Inaelezwa, sokoni hapo mchele unauzwa kwa bei ya Shilingi 2,300 hadi Shilingi 3,000 kutegemeana na aina yake na upo wa kutosha sanjari na bidhaa zingine.
Kwa upande wake, Mwenezi Khamis Mbeto aliwataka wananchi kupuuza maneno ya mtaani kwamba, bidhaa zimepanda bei sababu ya SMZ kuchelewesha baadhi ya meli kushusha mizigo bandarini, madai ambayo hayana ukweli.
Kabla ya kuanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Hussein Mwinyi alikagua bidhaa za vyakula katika masoko mbalimbali na kuridhishwa upatikanaji wake na kuwataka na kuwataka wafanyabiashara kutoongeza bei.