Na Beatrice Sanga, MAELEZO
WAKATI akihutubia katika hafla ya utiaji saini mkataba hodhi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki litakalo jengwa kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya mafuta ya ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP), Rais Samia Suluhu Hassan alionesha imani kuwa, mradi huo utachochea juhudi za pamoja za utafutaji mafuta na gesi katika nchi za ukanda huu zikiwemo Tanzania, DRC, Burundi na Sudan Kusini na pia utawavutia wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza Tanzania na nchi nyingine katika ukanda huu.
“Ujenzi wa bomba hilo utachochea utafutaji wa mafuta wa pamoja katika eneo la Afrika Mashariki na unatarajiwa kukuza sekta ya utalii, kilimo biashara na usafirishaji na utafiti wa rasilimali mafuta kwa nchi nyingine za Afrika”, alisema Rais Samia.
Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema, moja ya changamoto kubwa alizoziona katika safari yake ya kupigania ukombozi na maendeleo ya Afrika ni kukosekana kwa mwelekeo, lakini kuanza kwa mradi huu ni uthibitisho kuwa sasa mwelekeo unaonekana.
Ni miaka takribani mitatu sasa imepita tangu kuwekwa kwa jiwe la ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania. Mradi huo utagharimu Dola za Marekani Bilioni 3.55/- na unatarajiwa kusafirisha mapipa laki 2 ya mafuta kwa siku na wakati wa ujenzi ajira kati ya 6,000 mpaka 10,000 zitazalishwa.
Kwa sasa Serikali za Uganda na Tanzania pamoja na kampuni ya mafuta ya Total ya Ufaransa na Sinoc ya China kwa kushirikiana na Mashirika yanayohusika uzalishaji mafuta ya Tanzania na Uganda, zimeshasaini mikataba na ujenzi utaanza mara moja.
Katika mikataba hiyo nchi za Tanzania na Uganda kila moja inamiliki asilimia 15 ya hisa zote za kampuni hiyo, na kutokana na umiliki huo Tanzania itapata asilimia 60 ya mapato na Uganda itapata asilimia 40 zitakazotokana na mapato ya Dola za Marekani Milioni 290 zinazotarajiwa katika kipindi cha miaka 25 ya uhai wa mradi huo. Tanzania itapata mapato ya Dola za Marekani milioni 73, fedha za kigeni zitaongezeka kwa asilimia 53 na ajira zaidi ya 10,000 katika mikoa 8, Wilaya 24, Kata 134, vijiji 257, na vitongoji 527 ambako bomba litapita.
Ujenzi wa mradi huo ni kielelezo tosha cha ushirikiano wa Tanzania na Uganda kwani taarifa zinaeleza kuwa mradi huo ulipaswa kujengwa kupitia bandari ya Lamu nchini Kenya. Hata hivyo, viongozi wa Tanzania na Uganda wanaamini kwamba utulivu wa kisiasa, usalama na uzoefu wa kuendesha miradi ya kusafirishaji mafuta ndiyo sababu iliyofanya mradi huu kujengwa nchini Tanzania
Aidha, Tanzania ina uzoefu wa muda mrefu katika utekelezaji, ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) lililojengwa mwaka 1968, likitoka Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia. Bomba la TAZAMA lina kipenyo cha inchi 8 mpaka 12 na urefu wa Kilometa 1,710, kati ya hizo Kilometa 860 zipo kwenye ardhi ya Tanzania na limekuwa likipitisha mafuta Tani Milioni 1.1 kwa mwaka.
Tanzania pia ina sifa ya uzoefu wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa bomba la gesi kutoka Songo Songo mpaka Dar es Salaam, lenye kipenyo cha nchi 12 na urefu wa Kilometa 25 kutoka kisiwa cha Songo Songo mpaka Somangafungu. Pia, kuna bomba lingine la urefu wa Kilometa 207 na kipenyo cha inchi 16, kutoka Somangafungu mpaka Ubungo Dar es Salaam, mbali na bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es Salaam lenye zaidi ya Kilometa 490.
Aidha, kuna bomba la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Mtwara, lenye urefu wa Kilometa 27 na kipenyo cha inchi 8, ambalo limeanza kutumika tangu 2006. Haya yote yanatajwa kusababisha mradi huu kujengwa katika ardhi ya Tanzania. Hatua hizi zote zinadhihirisha ushirikiano wa kibiashara uliopo kati ya Tanzania na Uganda na nchi zingine za jirani katika kujenga uchumi kwa nchi zote.