TIMU ya Mkoa wa Mwanza imeanza vizuri mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa shule za Msingi UMITASHUMTA katika mchezo wa Netiboli, baada ya kuibuka mshindi dhidi ya Rukwa.
Katika mchezo uliochezwa leo asubuhi Juni 10, 2025, kwenye viwanja vya chuo cha ualimu Kleruu, Mabingwa watetezi Mwanza waliifunga Rukwa kwa magoli 55 kwa 10.
Mchezo mwingine wa kusisimua uliochezwa kwenye uwanja huohuo, ulimalizika kwa timu ya Mkoa wa Songwe kuifunga Katavi kwa magoli 54-6.
Mkoa wa Tabora ambao ulikuwa mwenyeji wa UMITASHUMTA& UMISSETA kwa mwaka uliopita, ulianza mashindano ya mwaka huu kwa ushindi wa magoli 21 kwa 18 dhidi ya timu ya Mkoa wa Kagera.
Kwa upande wa Singida walipoteza mchezo wao wa kwanza mwaka huu, baada ya kukubali kipigo cha magoli 57 kwa 5 kutoka Mkoa wa Geita.
Mratibu wa mchezo wa Netibali katika UMITASHUMTA ya mwaka huu Stella Mwangomale, amesema kuwa timu zimeanza vizuri na wanategemea ushindani mkubwa mwaka huu kutokana na mikoa kuonekana kujiandaa vizuri.
“Kuna jumla ya timu 26 zinazoshiriki Netiboli mwaka huu, zote zimejiandaa vizuri na tunatarajia ushindani wa hali ya juu pengine kuliko hata mwaka uliopita kule Tabora” amesema Mwangomale.
UMITASHUMTA & UMISSETA inaandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utamaduni na Michezo.