Na ORCI, Dar es Salaam
WAGONJWA wa saratani pamoja na ndugu zao walioambatana, wakiwasindikiza kupata matibabu ndani ya Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) wameanza kupatiwa elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage, akizungumza na wagonjwa na ndugu hao alisema, iwapo kila Mtanzania atakuwa na bima ya afya, itaondoa changamoto ya kukosa huduma kwa sababu ya kikwazo cha ukosefu wa fedha kutoka mfukoni.
“Muswada Bima ya Afya kwa Wote uliwasilishwa kwa mara ya kwanza Bungeni Septemba, mwaka huu na utawasilishwa tena mwezi Novemba.
“Tunafahamu inahitaji wananchi wote waweze kupata bima hii ili wanapofika hospitalini kwetu wapate huduma bila kuwepo jitihada za kutoa fedha mfukoni,” alisema.
Aliongeza: “Tunafahamu huduma za saratani ni ghali kwa wastani mgonjwa mmoja gharama yake kumtibu ni kati ya Shilingi Milioni 5 hadi Milioni 8 na hii ni kwa saratani ya kawaida (wengi hawamudu gharama) ndiyo maana huduma hizi serikali inatoa bure (akifika Ocean Road).
“Lakini tukiwa na bima ya afya kwa wote, hata kule kwenye ngazi za awali kwenye hospitali za wilaya, mikoa na Taifa ambako zinagundulika, mgonjwa hatalazimika kuchangia tena kupata huduma zile.
“Kwa sababu ili kupata huduma za saratani lazima ufanyiwe uchunguzi ithibitike una saratani na ukifika kwetu huduma bure lakini ngazi zingine kule kote anachangia mpaka ugonjwa uthibitike.
“Nimewaelekeza (wagonjwa na ndugu zao kwamba) wakiwa na kadi za bima ya afya kwenye hatua zote hizi hatatoa hela mfukoni bima yake itamsaidia kupata hizi huduma.
Dkt. Mwaiselage alifafanua: “Tumeona changamoto wagonjwa wetu wanachelewa kufika hospitali kwetu na hata wakifika ugonjwa unakuwa hatua za juu.
Alisema, upo utafiti ambao ulifanyika na kuonesha mgonjwa mmoja wa saratani huchukua takriban miezi tisa hadi kufika Ocean Road na wengi wao hufika wakiwa hatua za juu za ugonjwa.
“Inawezekana alienda wilaya inabidi achangie hana bima anaambiwa labda alipie xray, kipimo cha damu, anarudi kijiji anakaa huko wiki moja hadi mbili, achangiwe hela ndiyo akapime.
“Bima ya Afya kwa Wote itakuwa mkombozi kwa wananchi kufika mapema wataweza kutibiwa na kupona saratani zao,” alisisitiza.
Aliongeza: “Tumewapa elimu wagonjwa na ndugu za wagonjwa ili ikija wawe na mtizamo chanya gharama si kubwa sana Shilingi 340,000 watu sita na mmoja ni 84,000 ni nafuu.
“Tunatumia gharama kubwa sana kulipia mambo mengine kuliko afya zetu, wananchi wengi wametaka ziharakishwe kwa sababu ni mkombozi, wanataka iharakishwe ianze kwa haraka,” alisema.
Dkt. Mwaiselage alisema, Bima ya Afya kwa Wote itakapoanza Tanzania hospitali zote zinazotoa huduma na taasisi zote zinazotoa huduma za bima ya afya zitakuwa chini ya usimamizi madhubuti wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA).
“Itakuwa chini ya udhibiti wa TIRA…tunajua (TIRA) ilikuwa inadhibiti bima nyingine za magari, maisha, nyumba ilikuwa inadhibiti lakini bima ya afya ilikuwa inadhibitiwa na mifuko ya jamii, kuanzia hapo itadhibitiwa na TIRA.
“Inamaanisha makampuni yote yatakayoanzishwa na yatakayokuwapo itakuwa chini ya hii mamlaka hata hospitali zetu tutakuwa chini ya ofisi hiyo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa ni kupitia vigezo na vifurushi ili kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisisitiza.
Akitoa maoni yake mwananchi, Wallace Mnkande alisema ni hatua nzuri Tanzania kuelekea Bima ya Afya kwa Wote huku akitoa rai kwa hospitali na watoa huduma kuhakikisha zinaboresha mapema huduma zao ili kuepusha kero na malalamiko pindi tu itakapoanza.
“Tumemsikiliza Mkurugenzi ni mawazo mazuri, Serikali iwe imejipanga vya kutosha mtu akitibiwa anayetoa huduma ya bima walipwe kwa wakati vinginevyo mtu atachukua ‘cash’.” alisema.
Alishauri Serikali iweke angalau kipindi cha miezi mitatu mitatu kwa mwananchi kulipia bima yake na si mara moja kwa mkupuo mmoja. “Angalau tuseme kila baada ya robo mwaka alipie,”
Naye Zainab Mtubu ambaye anauguza mjomba wake hospitalini hapo alisema, iwapo Tanzania itafikia Bima ya Afya kwa Wote itakuwa mkombozi wa uchumi na uhusiano mwema ndani ya familia na ukoo.
“Bima ya Afya kwa Wote itafanya hata ukoo uwe karibu sasa hivi ukiambiwa una saratani ukoo unakukimbia, nimeachwa mwenyewe na mgonjwa, watu wanaona imekwisha.
Aliongeza: “Hiyo bima ifanyiwe haraka kuanza tumeambiwa hadi mwezi wa saba, lakini naona ni mbali ije haraka, kwa sababu nikitoa 340,000 kwa watu sita, kama sisi wengine hatuugui itamsaidia atakayeugua kati yetu,
“Tunaumia wananchi, hii kitu (muswada) kama inaenda huko bungeni iwe kitu ya kwanza, mimi hapa ninavyoona naweza kumuacha mgonjwa wangu maana kiuchumi imeniathiri.
“Kutwa nzima nipo hospitali, saa ngapi nitaenda kwenye shughuli zangu, lakini nikimuacha hapa nitaonekana mbaya zaidi kwenye ukoo kutokana na kwamba nilitafuta hili jambo na nimeshindwa kulimaliza.
“Lakini ni zito siwezi kulibeba mwenyewe, nina watoto wangu … ikija (Bima ya Afya kwa Wote) tutajua kuna hiyo 340,000, tulipe lakini pia huduma ziwepo lakini siyo tena iwe changamoto kupata huduma bora,” alitoa rai.