Bilioni 4.6 kupeleka umeme maeneo ya migodi Ruvuma

0

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali imetenga takribani Shilingi Bilioni 4.6 kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi mkoani Ruvuma.

Kapinga ameyasema hayo Agosti 18, 2024 wakati akizindua Kituo cha Mauzo ya Makaa ya Mawe ya kampuni ya Market Insight Limited (MILCOAL), inayojihusisha na uchimbaji, uuzaji na usambazaji wa Makaa ya Mawe, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

“Hapa katika mgodi wa MILCOAL tutatumia takribani Shilingi Milioni 280 kuleta umeme, nguzo tayari zimeshawekwa na sasa hivi wataalam wameanza kazi ya kuvuta waya,” alisema Kapinga.

Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Nishati inatekeleza miradi ya kupeleka nishati ya umeme kwenye maeneo makubwa ya uwekezaji ikiwemo migodini.

Kapinga alisisitiza, makaa ya mawe ni chanzo cha nishati thabiti na ya kutegemewa katika maeneo ya uwekezaji mkubwa hususani viwandani.

Aliwapongeza MILCOAL kwa uwekezaji huo ambao unachangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwahakikishia wawekezaji kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inathamini wawekezaji.

Kuhusu Kampuni kuwajibika kwa jamii inayozunguka miradi kwa maana ya CSR, Kapinga alisema Sera za Nishati na Madini zinatambua uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii zinazozunguka miradi na hivyo ameitaka Kampuni ya MILCOAL kutekeleza suala hilo ipasavyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here