Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya Shilingi Bilioni 28, zimetumika kwa ajili ya kuboresha kujenga miundo mbinu inayoipa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission – TAEC) uwezo wa kutoa huduma kwa tija na ufanisi.
TAEC ilianzishwa kwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano Na.7 ya mwaka 2003 (The Atomic Energy Act, No. 7 of 2003) ikiwa na majukumu makubwa mawili; kudhibiti matumizi salama ya mionzi na kuinua matumizi salama ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Lazaro Busagala akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya habari alisema, Serikali imejenga majengo sita (6) ya maaabara na ofisi katika Kanda 5 yenye thamani ya takribani Bilioni 28.11, ambapo majengo manne (4) kati ya hayo yamekamilika.
“Miradi hiyo ipo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na jitihada za kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao kwa kufungua ofisi,” alisema Prof. Busagala.
Aidha, alisema katika miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ofisi 14 zimefunguliwa na kuwekewa vitendea kazi, hivyo kuzifanya kuwa 63 mipakani na mikoani. “Lengo ni kusogeza huduma kwa wananchi hivyo kuinua shughuli za kiuchumi za wananchi.”
Kutokana na maboresho hayo yaliyofanyika, Makusanyo ya maduhuli ya Serikali yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 8.7 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Shilingi Bilioni 10.9 bilioni mwaka wa fedha 2022/2023.
“Mafanikio haya yametokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kufungua ofisi za Kanda, mipakani na kutumia mifumo ya TEHAMA kama vile TANCIS, TeSWS na EDMS katika kutoa huduma,” alisema Prof. Busagala.