WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mohamed Mchemgerwa amesema Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 18 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya TEHAMA, ambapo kupitia Programu ya SEQUIP, Shule za Sekondari 1,500 zinatarajiwa kunufaika.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa Shule za Sekondari nchini iliyofanyika katika Shule Maalum ya Wasichana ya Sayansi ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyopo Manispaa ya Ubungo, Mchengerwa amesema vifaa hivyo vinalenga kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa njia ya kisasa kwa kutumia na kujifunza TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia Duniani.
Alisema, matumizi ya vifaa vya TEHAMA ni moja ya afua na viashiria vya utekelezaji wa mradi wa SEQUIP inayolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kupitia TEHAMA katika Shule za Sekondari.
Kupitia utekelezaji wa mradi wa SEQUIP jumla ya Shule za Sekondari 1,500 zinatarajiwa kunufaika kwa kupata vifaa vya TEHAMA. Kwa leo hapa tunatoa vifaa kwa shule 231 ambazo ni sehemu ya shule hizo 1,500 zitakazonufaika na mpango huu.
Katika kufanikisha azima hii, Serikali ilianza kutoa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA na huduma ndongondogo ya vifaa hivyo kwa walimu 3,132 wa Shule za Sekondari.
Utoaji wa mafunzo kwa walimu hawa unalenga kuhakikisha walimu wamejengewa uwezo katika kutunza Vifaa vilivyonunuliwa, kutumia vifaa kwa ufasaha ikiwemo kuwaelekeza wanafunzi na kufanya huduma ndogondogo inapotokea hitilafu katika vifaa husika.
Aliongeza kuwa, manunuzi ya vifaa vya TEHAMA yamezingatia mwongozo wa SEQUIP ( ICT package) kwa kila Shule ya Sekondari inayonufaika. Kufuatia mwongozo huo vifaa vilivyonunuliwa ni Kompyuta za mezani 1,848, UPS 462, Kompyuta Mpakato 231, Projekta 231 na Projekta “screen” 231
Serikali inaamini kuwa, Matumizi ya vifaa vya TEHAMA ambavyo usambazaji wake unazinduliwa leo yataleta mapinduzi makubwa katika ujifunzaji na ufundishaji katika Shule za Sekondari.
Kupitia vifaa hivi, walimu wataongeza ufanisi katika ufundishaji na wanafunzi watapata maarifa ya ziada wakati wa kujifunza.