Benjamin Kamtawa (kulia) akimkabidhi Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Juma Nambaila, fomu ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho, unaotarajia kufanyika hivi karibuni.
Na Mwandishi Wetu
MWANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Magnus Kamtawa ni miongoni mwa waliotia nia ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa Jimbo la Peramiho, kwenye uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika hivi karibuni.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jenista Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, 2025 jijini Dodoma kutokana na maradhi ya moyo, na kuzikwa Desemba 16, 2026 katika Kijiji cha Luanda, kilichopo Wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu jana Januari 19, 2026 Kamtawa alisema, iwapo atapata ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi huo na kupata nafasi ya kuwa mbunge wa Jimbo hilo, ataendeleza alipoishia Jenista kwa kusimamia kwa uaminifu mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya 2025–2030.
Kamtawa alisema, kuna mambo ambayo Jenista alikuwa anayatekeleza kwa niaba ya chama kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa Jimbo la Peramiho, hivyo iwapo atapata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo, ataendeleza alipoishia mbunge huyo.
“Dada yetu Jenista kwa kipindi chote alichokuwa mbunge alikuwa anasimama Ilani ya chama, namimi nimeona nijitokeze kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa Jimbo letu ili niendelee pale alipoishia katika kutekeleza Ilani ya CCM,” alisema Kamtawa.
Alisema, zipo changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zinafanyiwa kazi likiwemo suala la miundombinu ya barabara, ambapo Ilani ya CCM imeendelea kulipa kipaumbele suala hilo, hivyo akipata nafasi ya kuwa mbunge, atalisimamia kwa nguvu zote.
“Wananchi wa Peramiho wanahitaji huduma bora za afya, elimu na mengineyo na yote haya yapo kwenye Ilani ya chama chetu cha Mapinduzi, mimi nipo tayari kuyasimamia nikipata nafasi ya kuwa mbunge kwa kushirikiana na wananchi wenzangu wa Jimbo la Peramiho,” alisema Kamtawa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya maktaba, pia ana digrii ya Uzamili ya usimamizi wa biashara na masoko.
Mchakato wa kumpata mrithi wa Marehemu Jenista Mhagama, ulianza Januari 18, 2026 na umehitimishwa Januari 19, 2026, ambapo wanachama takribani 27 wa Chama cha Mapinduzi wamechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.