Bashungwa atoa mwezi mmoja….

0
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa mwezi mmoja kwa Kamati inayoandaa Mkakati wa kuongeza ushiriki wa Wazawa katika Miradi ya Ujenzi kukamilisha maboresho ya taarifa hiyo ili iweze kubeba maudhui yote ya Sekta ya Ujenzi na kuweza kuleta tija kwa nchi.

Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma katika kikao kazi cha uwasilishaji wa taarifa hiyo na kusisitiza kwa Kamati kuangalia maeneo muhimu ikiwemo uandaaji wa nyaraka za zabuni, vigezo vya upataji wa miradi, mikataba na masuala ya Kisheria.

“Fanyeni tafiti kujua nchi nyingine zimefanikiwa vipi katika suala la kuwajengea uwezo wataalam wao (Local Content), hakikisheni ripoti ya mwisho inafikisha matarajio yote ya wataalam wa Sekta ya Ujenzi”, alisema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesisitiza umuhimu wa mkakati huo katika kuongeza wigo wa kuwajengea uwezo Wataalam wa Sekta ya Ujenzi nchini ili kuhakikisha utalaam na ujuzi unakuzwa kwa maendeleo ya nchi.

Bashungwa ameelezea umuhimu wa ushirikishwaji wa Wazawa katika nchi ikiwemo fedha nyingi kubaki nchini na kukuza biashara za wazawa, kuongeza ajira na ujuzi kwa wataalam wa ndani, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kujenga makampuni ya ndani kuwa makubwa na yenye uwezo wa kushindana kimataifa.

Bashungwa alisema, taarifa hiyo pia iweke mazingira wezeshi ya kusaidia wakandarasi wazawa kutekeleza miradi kwa kuwa Serikali imeweka kwenye sheria kiwango cha thamani ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa na wazawa kutoka Shilingi Bilioni 10 hadi Bilioni 50 ili kuwawezesha wazawa kunufaika na miradi hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Matiko Mturi ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), amemhakikishia Waziri huyo kuwa kwa kushirikiana na wadau wote wataendelea kukusanya maoni ili mkakati huo uwe na manufaa kwa pande zote na usaidie katika kukuza uchumi wa nchi.

Aliongeza kuwa, miradi ya ujenzi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia Januari 2013 hadi Juni 2023 ni 36,839 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 61.6 ambayo ilisajiliwa.

Kamati ya uaandaji wa Mkakati wa Ushiriki wa Wazawa katika miradi ya ujenzi imehusisha Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here