MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Abiria Maruhubi na Bandari Kavu ya Mpigaduri kutaiwezesha Zanzibar kufungua milango zaidi ya kiuchumi, pamoja na kuondoa changamoto katika sekta ya usafirishaji.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Hemed alisema kuwa bandari ni lango muhimu la uchumi kwa mataifa ya visiwani kama Zanzibar, na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha biashara na kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Malindi.
“Changamoto ya msongamano wa makontena na meli kukaa nangani kwa muda mrefu katika Bandari ya Malindi itakuwa historia. Serikali itahakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati,” alisema Hemed.
Aidha, aliagiza Shirika la Bandari Zanzibar kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa bandari hizo na kuwataka wananchi wa Chumbuni na maeneo jirani kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili kazi ikamilike kwa muda uliopangwa.
Hemed pia aliwahimiza wazawa kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye miradi hiyo, akisisitiza kuwa serikali inawapa kipaumbele Wazanzibari katika uwekezaji wa kimkakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, alisema kuwa ujenzi wa bandari ya abiria Maruhubi utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 400, na utahusisha jengo la kisasa la abiria, eneo la kutua ndege, kituo cha mabasi, pamoja na uwezo wa kuhudumia meli nne kwa wakati mmoja.
“Bandari hii itaweza kuhudumia abiria zaidi ya milioni tano kwa mwaka na itakuwa na teknolojia ya kuzalisha nishati, jambo litakalosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira,” alisema Akif.
Mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kampuni ya ZF Devco, ambayo itajenga na kuiendesha bandari hiyo kwa muda wa miaka 33.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa bandari ya abiria Maruhubi pamoja na bandari kavu ya Mpigaduri inatarajiwa kukamilika Oktoba 2025, huku awamu ya pili kwa ajili ya boti za mwendokasi ikitarajiwa kukamilika mwaka 2027.