KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amehitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma, akisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa chama cha wanachama, kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote na kuwa mtetezi wa wanyonge.
Balozi Nchimbi alisema kwamba katika kuendeleza nafasi yake kama taasisi imara inayohusika na uongozi wa nchi, CCM hakina budi kuendeleza misingi ya sera zake zinazolenga kubadilisha hali za maisha ya watu, kuendana na mahitaji ya nyakati, na kuzingatia maslahi ya taifa.

Dkt. Nchimbi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanaCCM na wananchi wa mji wa Songea, waliokusanyika kumpokea alipofika kufungua mradi wa kitega uchumi wa Tawi la CCM la Mshangano mjini Songea, Jumapili tarehe 6 Aprili 2025, ikiwa ni siku ya tano tangu alipoanza ziara hiyo tarehe 2 Aprili 2025.
Katika ziara hiyo aliyoanzia katika Wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Nyasa, na hatimaye Songea mjini, Balozi Nchimbi alitoa pongezi kwa Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kwa jinsi inavyotafsiri kwa vitendo na ufanisi, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, kupitia miradi ya maendeleo na huduma kwa wananchi.

Balozi Nchimbi alitoa maelekezo kwa Serikali kuendelea kusimamia na kubuni mipango inayolenga kuongeza matokeo chanya kwenye shughuli za uzalishaji mali, ikiwemo kilimo na madini, ili wakulima na wachimbaji madini waendelee kuzalisha kwa tija itakayoongeza pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Balozi Nchimbi alitembelea na kutoa maelekezo mahsusi katika miradi kadhaa ya maendeleo na ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia wizara na taasisi zake, ikiwemo mradi wa uzalishaji mbegu chini ya Mamlaka ya Mbegu Nchini (ASA) na ujenzi wa Bandari ya Nyasa, kwa lengo la kuendelea kutafsiri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Katika mikutano ya hadhara katika wilaya mbalimbali, pamoja na kusalimia wananchi katika maeneo ya Songea Vijijini, Mbinga na Songea mjini, Balozi Nchimbi alipokea taarifa za utendaji wa kazi kutoka kwa viongozi wa Chama na Serikali, na pia alipokea maoni ya wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili, kupitia kwa wabunge na wananchi moja kwa moja, kisha kutoa maelekezo ya kutatuliwa kwa kero hizo.
Balozi Nchimbi, ambaye amehitimisha rasmi ziara yake kwa kuondoka mkoani humo Jumatatu tarehe 7 Aprili 2025, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wanaCCM na Watanzania wote kwa ujumla kwa ushirikiano wao na Serikali ya CCM katika kulinda tunu za taifa, ikiwemo amani na utulivu. Alitoa wito wa kuendeleza hali hiyo wakati nchi inapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.