Angela Msimbira OR-TAMISEMI
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde amewapongeza viongozi pamoja na watendaji wa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kwa kufanya vyema kwenye ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi.
Ameyasema hayo kwenye kikao kazi cha maofisa elimu kata, wakuu wa shule na walimu wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Amewataka kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuinua kiwango cha elimu kwa upande wa shule za sekondari katika halmashauri hiyo ili kuleta uwiano sawa na kuinua kiqango cha elimu katika halmashauri hiyo.
Dkt. Msonde alisema, Idara ya Shule za Msingi inafanya viizuri sana katika mitihani yao, lakini ulipofanyika uchambuzi wa ufaulu wa kidato cha pili na kidato cha nne, Bahi haikufanya vizuri kwenye matokeo ya mwisho, hali aliyosema haridhishi na kunahitajika kuweka mikakati ya kuinua kiwango cha elimu kwa upande wa elimu ya sekondari.
Ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha inajiwekea mikakati madhubuti ya kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa shule za sekondari iwe kitovu cha elimu ambako watu wengine wataenda kujifunza.
“Sisi sote tuna wajibu wa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan hivyo tuna wajibu wa kujitoa kwa hali na mali katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya elimu kwa kuhakikisha tunatumia mbinu mahususi za kuwafundisha watoto ili waweze kupata uelewa, ujuzi na maarifa,” alisema Dkt. Msonde.
Dkt. Msonde alisema mwalimu ni mlezi na nidhamu na tabia ya mtu hutengenezwa kuanzia ngazi ya utotoni hivyo ni wajibu wa mwalimu kutoa ujuzi na maarifa ili kumwezesha kuweza kufikia malengo na kuleta maendeleo binafsikwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Taifa lolote linasimamishwa na mwalimu, hivyo anahitaji heshima hadhi kupendwa na kiwa moyo kutokana na wajibu wake kwa jamii,” alisema Dkt. Msonde.