Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, kimesema uamuzi wa ACT Wazalendo kuitangazia Dunia kuwa inashiriki kikamilifu Uchaguzi Mkuu 2025, iwe somo kwa Chadema.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Zanzibar, Mbeto alisema suala la uchaguzi sio la chama cha siasa ni haki ya wananchi kushiriki na mpango wa ‘No Reform No, Election’ unawanyima haki yao.
Alisema, ACT Wazalendo wengi wao walikuwa CUF wanajua athari za kususia uchaguzi ndio maana wameamua kushiriki kikamilifu kwa kusimamisha wagombea katika nafasi zote za Ubunge, Udiwani na Uwakilishi.
“Wamesha soma, kuna viongiozi wa ACT Wazalendo walipokuwa CUF, wakasusia uchaguzi 2015 wa marejeo waliona, walikosa uwakilishi wa wananchi katika maeneo mengi,” alisema.
Mbetto alibainisha kuwa, wao kama wadau wa uchaguzi wameona jambo jema walilofanya ACT Wazalendo ingawa ipo wazi kuwa CCM itapata ushindi wa kishindo.
Alisema, kazi iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi ndio zitakazo wafanye ACT kushindwa vibaya.
“Uchaguzi ni fursa, watapata Uwakilishi, Udiwani na Ubunge tofauti na Chadema ambao itabidi wasubiri baada ya miaka mitano,” alisema.
Mbeto alisema, mwaka 2015 CUF walisusia uchaguzi mkuu wa marudio na matokeo yake wananchi wengi ambao ni wanachama wao walikosa haki yao ya kuushiriki.
Alisema, chama kukaa miaka mitano bila kushiriki siasa ni wazi kuwa kitakufa, hivyo anawataka wananchi wasipoteze haki yao ya kushiriki uchaguzi wahamie vyama vingine vya siasa.
“Unapokiondosha chama kwa miaka mitano automatically chama unaenda kukiua, uhai wa vyama cha kisiasa ni kuwepo katika Bunge na Uwakilishi,” alisema.
Mbeto anawasihi, watanzania wenye nia ya kutaka kupata ridhaa kupitia vyama vya siasa kutaka kugombea, wachangamkie fursa kwa kujiunga na vyama vingine.
“Kama mlango wa kushoto umefungwa, basi tafuta wa kulia hivyo wajiongeze na kwa kuwa kugombea lazima upitie chama cha siasa, nchini kuna vyama 19,”
“Hivyo wale ambao wamenyimwa haki hiyo wanaweza kwenda kujiunga vyama vingine na CCM huwa inafurahi inapokuwa katika Bunge na Baraza la Wawakilishi na upinzani kwani inapanua wigo wa mijadala” anasema.
Mwenezi huyo anabainisha kuwa CCM haina urasimu wa kutaka kuhodhi madaraka na ndio maana wanautaka upinzani Bungeni na Baraza la Wawakilishi.
Mwenezi huyo anawashangaa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na Makamu wake John Heche wanaodai bila mabadiliko hakuna uchaguzi.
“Mwaka 2015 walishinda Ubunge kwa zaidi ya vipindi viwili, chini ya Tume ya Uchaguzi, katiba na sheria zilizopo hivisasa,’’ alisema Mbeto.
Alisema, mbali na hilo pia walikusanya asilimia 42 ya kura za Urais na viti vingi vya Ubunge na Udiwani katika miji takribani yote mikubwa “wakati huo yote hawakuyaona?”
Mwenezi Mbeto alisema, Watanzania wanataka zaidi amani, utulivu pia wanahitaji kusikilizwa na kuchagua viongozi kwa mujibu wa katiba.