SMZ kuendelea kujenga nyumba bora za kisasa

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kujenga nyumba bora za kisasa za makazi, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata makazi yaliyo salama na yenye staha.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipozindua mfumo wa kidijitali wa utoaji huduma pamoja na uzinduzi wa mauzo wa Mradi wa Nyumba za Kisasa Mwinyi Housing Scheme, hafla iliyofanyika katika Hoteli ya New Amaan, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mei 10, 2025.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alisema, Serikali inalenga kuweka mpango mahsusi wa kuwawezesha wafanyakazi wenye kipato cha chini kununua nyumba bora za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar.

Alibainisha kuwa, mpango huo utakuwa na makato madogo ya marejesho, ili kuwawezesha wafanyakazi hao kumiliki nyumba bora kwa gharama nafuu.

Alisisitiza, ni jukumu la msingi la Serikali kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira bora na salama ya makazi.

Rais Dkt. Mwinyi pia alisema, Serikali itaendelea kujenga nyumba za kisasa kwa lengo la kuimarisha muonekano na haiba ya miji nchini.

Aidha, amelipongeza Shirika la Nyumba kwa mafanikio makubwa linayoyapata hivi sasa, yakiwemo uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa ZHC Connect App, ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa za huduma zinazotolewa na shirika hilo.

Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba 3,000 za makazi katika eneo la Chumbuni, ambapo nyumba 1,095 zinajengwa kwa awamu ya kwanza.

Mradi wa Mwinyi Housing Scheme utaanza katika eneo la Kisasaka kwa ujenzi wa nyumba 520, ambao ndio uliyozinduliwa rasmi.

Rais Dkt. Mwinyi alitoa wito kwa wananchi kununua nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba katika maeneo mbalimbali yenye hadhi nchini, amesisitiza kuwa ni fursa ya kipekee ya kumiliki makazi bora kwa gharama nafuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here