SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya mashine aina ya msumeno mnyororo (chain saw) kukatia miti bila kibali kutoka mamlaka husika ili kupunguza kasi ya uharibifu wa uoto wa asili na mazingira kwa ujumla.
Sanjari na hilo pia imesema katika kukabiliana na janga la ukataji holela wa miti, hekta takribani Milioni 5.2 za maeneo yaliyoharibiwa zinatarajiwa kupandwa miti ifikapo mwaka 2030.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema hayo leo Mei 5, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) lililoulizwa na Mbunge wa Moshi Vijijini Prof. Patrick Alois Ndakidemi aliyetaka kujua tamko la Serikali kwa watu wanaovuna miti kwa kutumia misumeno mnyororo na hivyo kuwa kikwazo katika juhudi za kuhifadhi mazingira.
Akiendelea kujibu swali hilo, Katambi alisema kuwa pamoja na kwamba mashine hizo zinauzwa nchini upo utaratibu maalumu unaotoa mwongozo wa kufuata zisitumike ovyo kwenye maeneo ambayo hayajatolewa vibali.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais nitoe maelekezo ni marufuku kwa mtu yeyote kutumia chain saw bila kibali kutoka mamlaka zilizopo kwenye maeneo husika inayotambulika kisheria, kuna utaratibu wa namna ya kufanya uvunaji, tunaomba wazingatie hili kwani kwa ukiukaji wa taratibu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.
Aidha, akijibu swali la msingi kuhusu upi mpango wa taifa wa kupanda miti kwa kipindi cha muda mfupi na mrefu ili kukabiliana na janga la kukata miti, Katambi alibainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Maliasili na Utalii, inatekeleza mpango wa muda mrefu wa Mkakati wa kurejesha kwa kupanda miti maeneo yaliyoharibiwa.
Naibu Waziri Katambi alisema, katika mkakati huo miongoni mwa shughuli zinazoendelea ni pamoja nakuhamasisha wananchi kutunza mazingira kupitia kampeni za upandaji miti Milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa kila mwaka.