Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimewataka viongozi wa Dini kuendelea kuliinda misingi ya Umoja wa Kitaifa, kusimamia Amani na Utulivu kwakuwa Tanzania bila Amani haiwezi kusimama kwa nguvu zake.
Pia, chama hicho tawala kimewahimiza Viongozi wa Dini zote kupunguza majibizano yasiyo na Afya kwa ustawi na mustakabali wa maendeleo ya Taifa zima.
Ushauri huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis aliyesema Tanzania yetu iwe mbele kwanza kuliko imani na dini zetu.
Mbeto alisema, wakati huu Tanzania ikielekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba Mwaka huu, dini, kabila, kanda na nasaba zinaweza kutumiwa na wanasiasa ili kusaka kura jambo ambalo ni baya na hatari sana.
Alisema, endapo Viongozi wa madhehebu ya Dini hawatosimama imara, na kuwa wa kwanza kuwaonya waumini wao, Tanzania inaweza kujikuta ikipoteza sifa yake adhim ya kuwa kisiwa cha Amani.
“CCM kinawahimiza Viongozi wote wa dini kuacha kutoa matamshi makali yasio na afya kwa Taifa .Tanzania iwe kwanza kuliko imani na dini. Majibizano ya ana kwa ana hayajengi Umoja na maelewano thabiti,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliwataka Viongozi hao wa dini kukumbuka na kuenzi wasia wa Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, aliyeongoza Taifa letu kwa miaka 23 bila dini kujiingiza katika medani za Siasa na Utawala
“Utawala wa nchi yetu haujawahi kufungamana na dini yoyote. Mara zote na mahali popote Mwalimu Nyerere amekuwa akiamini katika dhana ya Umoja wa Kitaifa zaidi kuliko udini, ukanda na ukabila” alieleza.
Mbeto alisema, katika nyakati hizi kuelekea Uchaguzi Mkuu, watajitokeza baadhi ya Wanasiasa wanaotaka kura na kuwa viongozi kwa kutumia aidha ukabila, nasaba, udini au kwa rangi za asili yao.
“Viongozi wa Dini simameni kidete kulinda Taifa. Mawazo, fikra na mitazamo yenu ijielekeze zaidi katika utaifa kuliko dini zenu. Tanzania ina mengi ya kujifunza kutokana na matukio hatari kuwahi kutokea katika mataifa mengine duniani,” alisisitiza Mbeto.
Hata hivyo, Katibu huyo Mwenezi aliwashauri viongozi wa dini kutojihusisha na Siasa badala yake waendeleze kuhubiri Amani, Umoja na Utulivu. Bila kutumia hekima, busara na juhudi Taifa linaweza kutoweka.