MAKAMU wa Pili wa Rais wa ZanzibarHemed Suleiman Abdulla amesema Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kwani utajadili mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Alisema mkutano huo pia, utawaunganisha Waafrika zaidi ya Milioni 300 katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030 ili kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Barani Afrika.
Hemed alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar, Aprili 28, 2025.
Kadhalika, Makamu wa Pili wa Rais amewataka washiriki huo kuhakikisha mijadala yao inalenga zaidi kuangalia fursa na changamoto ambazo Afrika inakabiliana nazo hivyo ni muhimu wawetumie mkutano huo kuweka vipaumbele muhimu vya kimkakati vitakavyoisaidia Afrika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema athari za mabadilko ya tabianchi zimekuwa zikiongezeka na kuathiri nchi nyingi za Afrika na kusababisha kupungua kwa fedha za hali ya hewa jambo linaliochangia wazalishaji wakubwa wa gesijoto kujiondoa kutokana na changamoto hiyo.
Hemed alisema, pamoja na kuwa Afrika ina utajiri wa asili kama ukiwemo madini muhimu kwa teknolojia ya kijani kibichi bado zaidi ya Waafrika Milioni 600 hawana uwezo wa kupata nishati safi na nafuu jambo ambalo halikubaliki hivyo jitihada za haraka zinapaswa.
Aliongeza kuwa, Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake ili kuvutia wawekezaji hasa katika nishati ya kijani na teknolojia zinazosukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.