Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeutaka Upinzani kutozibeza Tume za Uchaguzi, INEC na ZEC na kudai si huru wakati Chadema na ACT Wazalendo vimekuwa vikiongeza idadi vya Viti vya Udiwani, Uwakilishi, Ubunge na kupata kura nyingi za urais.
CCM kimesema Tume hizo ziko huru na kutenda haki zikiongozwa na binadamu na kwamba Tume yoyote itakayoundwa kwa mfumo wowote, zitaendelea kuongozwa na binadamu si Malaika.
Hayo yamesema na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema madai ya upinzani kuhusu Tume za Uchaguzi hayana mantiki, mashiko na kukosa nguvu ya hoja.
Mbeto alisema, chati ya idadi ya Viti vilivyokwenda upinzani kuanzia Mwaka 1995 hadi 2020, imekuwa ikipanda katika Uchaguzi za Serikali za Mitaa, Udiwani, Uwakilishi ,Ubunge na kuongezeka kura za Urais.
Alisema, katika Uchaguzi Mkuu wa Kwanza Mwaka 1995, NCCR-MAGEUZI na CUF, vilipata Viti kwa uchaguzi wa Tanzania Zanzibar ambapo CCM mwaka huo ilipata Viti 24 na CUF 23 vya Ubunge na Uwakilishi.
“Nafikiri maana ya uwazi na demokrasia kwa upinzani hadi itangazwe CCM kimeshindwa kura za urais. Uchaguzi ni mchakato wa kukubalika kwa chama cha siasa na wananchi. CCM kina Mizizi mirefu, Nyenzo, Rasilimali Fedha na watu kuliko Upinzani,” alisema Mbeto.
Hivyo basi, Mwenezi huyo katika maelezo yake , alisema, haiwezekani vyama vilichosajiliwa Mwaka 1993 na kuendelea kama Chadema NCCR-MAGEUZI, CUF, ACT au CHAMA viwe na ubavu wa kukiangusha CCM.
“CCM ni jiti kubwa lenye Matawi mapana na Mizizi mirefu. Gogo na shina la mti wake halikatiki kirahisi . Kuchuana na CCM katika Uchaguzi kunahitajika upinzani wenye mbavu nene za kisiasa,” alisisitiza Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi akitoa mfano, alisema uchaguzi wa Mwaka 2015, Chadema kilipata Viti vya Ubunge maeneo ya Mijini na kukosa Vijijini, kutokana na uchanga wake kisiasa.
Mbeto alitaja kuna Wabunge wa Chadema wamekuwa bungeni kwa zaidi ya vipindi viwili, ushindi wao umetangazwa na Tume ambazo leo wanaibeza na kudai si huru.
“Kina Tundu Lissu, John Heche, John Mnyika, Godbless Lema, Halima Mdee, Ester Bulaya, Boniface Jackob, Peter Msigwa, Said Kubenea na Joseph Mbilinyi wote wametangazwa washindi na Tume ya uchaguzi iliyopo sasa,” alieleza Mwenezi huyo.
Akizungumzia Katiba ya Tanzania na Zanzibar, Mbeto alisema Katiba hizo, zimeongoza nchi kwa miaka 61 bila misukosuko ya aina yoyote, kila katika wakati mgumu Katiba hizo zilitoa majibu na kuelekeza.
“Serikali ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete iliunda Tume iliyokusanya maoni ya wananchi ilioongozwa na Joseph Warioba. Likaundwa Bunge Maalum la Katiba. Ilipoandikwa Katiba inayopendekezwa. Chadema na CUF wakawatoa wabunge wao kabla ya Bunge Maalum la Katiba hakijafikia tamati,” alisema.
Mbeto alieleza kuwa, leo unapoisoma Katiba iliyopendekezwa kwa utuo, utulivu na umakini, utaona ilivyozingatia changamoto na kutekeleza ushauri na maoni yaliyotolewa na watanzania kwa ustadi na mazingatio.