CCM: Muungano wa Tanzania utalindwa kwa nguvu zote

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema amani, usalama na utulivu wa Tanzania kwa miaka 61, umetokana na misuli ya ulinzi chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania..

Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Mbeto alisema, usalama na utulivu wa pande mbili za Muungano tokea mwaka 1961 kwa upande wa Tanganyika na Zanzibar kuanzia Mwaka 1964, baada ya hapo Muungano ndio unaosimamia maendeleo na Usalama wa Taifa.

Alisema, nje ya Muugano wa Tanzania, si Tanganyika wala Zanzibar ambazo zingeweza kuhimili harubu na misukosuko ya kusimamia ulinzi na usalama bila Muungano.

Alisema, wanaoshabikia na kutaka Muungano uvunjike; aidha watakuwa na ajenda za siri au ni vibaraka wanaotumiwa na maadui dhidi ya ustawi wa umoja na maendeleo.

Amewataka wanaotamka maneno hayo ni wazi watakuwa wameleweshwa na hali ya Utulivu na amani iliyopo kwa miaka mingi huku wakijua wanalindwa na Serikali ya Tanzania.

“Usalama wa Zanzibar na Tanganyika ni kutokana na Muungano. Nje ya Muungano hakuna Tanganyika wala Zanzibar, utachomoza ukabila na ubaguzi. Huyu Mpemba, yule Mu- Unguja, hawa wamehamia toka Oman na Bara na wale kule ni Wangazija na Wahindi,” alisema Mbeto.

Mwenezi huyo akitoa mfano, aliutaja Muungano wa nchi mbili za Tanzania si jambo geni duniani kwani kuna Muungano Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), wenye nchi nane.

Alizitaja nchi hizo ni Dubai Abu Dhabi, Sharjah na Ras al Hema.

Nyingine ni Ajman, Amulhuwein, Fujera na Olfaghan.

“Maendeleo ya UAE yametokana na Muungano, nchi nane zina Dola moja ya UAE na muungano huo ni mfano wa maendeleleo ya muungano duniani. Wanaoota Muungano wa Tanzania utavunjike watasubiri kwa miaka mingi “alieleza.

Alisema, Zanzibar imepata maendeleo ya ghafla baada ya ufalme kudondoka kwa miaka minane chini ya Rais Abeid Amani Karume, baada hapo tukaungana na wenzetu Tanganyika hadi sasa tunaishangaza dunia.

“Leo Zanzibar inatazamwa kivingine kwa maendeleo yaliotokea kwa miaka mitano ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi, baada ya miaka kumi Zanzibar itakuwa kama Dubai, Hong Kong au Singapore” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here