Mbeto: OMO asiwanie urais Z’bar kwa kutegemea hadithi za vijiweni

0

Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kutotia nia ya kuwania urais Zanzibar kwa kuziamini hadithi za kale za vijiweni na Mitaani zinazodai CCM hakijawahi kushinda.

Pia, CCM kimekumbusha asidhani kwa kulitumia jina la Hayati Maalim Seif Sharrif Hamad, kutamzidishia chochote ili akwepe kipigo cha kushindwa kwenye uchaguzi ujao.

Hayo yameeelzwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis aliyemtaka Othman, ajiandae kukumbwa na kimbunga kuliko kilichowahi kumkuta mgombea mwenzake wa upinzani.

Mbeto alimtaka OMO aache kuziamini hadithi zinazodai CCM hakijawahi kushinda wakati ushindi wake ndio unaounda Serikali toka mwaka 1995 hadi sasa huku yeye (Othman) akiwa sehemu ya watumishi chini ya SMZ.

Alisema, ni jambo la kushangaza kwa mtu mzima kama Othman kuamini CCM hakitashinda wakati Serikali ya CCM ndiyo inayomlipa mshahara, imekuwa akimpatia nyumba anayoishi na familia yake, magari, ulinzi na huduma nyingine muhimu.

“Othman jiandae kushindwa kama alivyoshindwa mgombea mwenzako kuanzia mwaka 1995 hadi 2020.

“Kila CCM iliposhinda na kuunda Serikali wewe umekuwa kati ya watumishi wake watiifu SMZ waliopatiwa ajira,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema, madai ya kuwepo uvunjaji wa haki za binadamu na kutofanyika mageuzi ya kiuchumi ni maneno yasioingia akili wakati Zanzibar ya leo ikiizidi kupaa kimaendeleo .

“Aache kuwania urais wa Zanzibar kwa kutegemea ubebwe na jina la marehemu.”

Mbeto alisema, Othman ameamua kuchukua fomu ya kuwania urais katika wakati ambao Zanzibar, chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imefanya mageuzi makubwa ya kimfumo, kitaasisi, kisheria na kuziweka sawa hali za maisha ya wananchi .

“Mgombea wa CCM hakumbushi tawala za kikoloni zilivyodumaza maendeleo ya Zanzibar. OMO anapokumbusha mambo yaliyojiri mwaka 1995 nae akiwa sehemu ya SMZ ni kukicheza shere chama chake,” alisema

Katibu huyo Mwenezi alibainisha kama kweli Othman anaamini CCM ilikuwa haishindi katika chaguzi zilizopita, mbona hakusita kukubali teuzi alizopata, akawa anakula viapo na kuitumikia SMZ kwa utii na uaminifu.

“OMO anasambaza upekepeke kuwa CCM haijashinda uchaguzi, wakati hakuwahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, si Mkurugenzi wala Mwenyekiti wa ZEC,” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here