Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitamvumilia hata kidogo mgombea yeyote wa chama hicho atakayejinadi akitumia ubaguzi wa aina yoyote ile.
Hayo yalisemwa na Katibu Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis katika mkutano na Wajumbe wa Kamati za Siasa na Utekelezaji za Matawi na Kata za Unguja, leo Aprili 16, 2025.
Mbeto alisema, yeyote atakayepitishwa au anataka kuwania nafasi yoyote, akijinadi kibaguzi hatavumiliwa.
“Mtu yeyote akijinadi kwa ukabila, ukanda ama kwa nafasi ya kwao, jina lake tutalikata mapema tu,” alisema Mwenezi huyo.
Alibainisha kuwa, CCM imeboresha mchakato wa kuwapata wagombea udiwani, Ubunge na wawakilishi ili kutoa nafasi kupatikana wigo mpana wa demokrasia tofauti na awali hivyo wakachague viongozi bora na sio bora viongozi.
“Awali wagombea walikuwa wanapigiwa kura ndani ya chama na Wajumbe Kamati Kuu ya Jimbo zikawepo kelele watu wachache kuwaamulia walio wengi sasa ni tofauti,” alisema,
Alibainisha kuwa, atakayepata nafasi akanadi sera za chama ili kujenga amani na mshikamano na sio vingine.
Mbeto ambaye amefahamisha mabadiliko ya siku za kuchukua fomu na kurudisha ambapo sasa kuanza kuchukua na kurudisha ni Juni 28 hadi Julai 2 alionya kuwa kuchukua sio ndio kampeni zimeamza.
“Ole wake mtu ndani ya kipindi hicho aanze kujinadi na kufanya kampeni, hatutamuelewa” alisema.
Amewataka kuchukua fomu kimya, kimya na kusubiri hadi Bunge na Baraza la Wawakilishi vitakapovunjwa.
“Baada ya vyombo hivyo kuvunjwa, Chama kitatoa mwongozo,” alisema Mwenezi Mbeto na kuongeza, “Tumeapa na tutatenda haki kwa mujibu wa mwongozo wa chama.”