Na Joseph Zablon
MBUNGE wa Konde, Pemba kwa tiketi ya ACT Wazalendo Mohamed Said Issa akiwa katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha ITV amesema, kelele alizokuwa anapiga kuhusu Hospitali, barabara, shule na miundombinu mingine yakiwemo maji zimetatuliwa.
Alisema, mara mbili kwa kutumia pesa zake alinunua gari la kusafirishia wagonjwa kuwapeleka hospitali pekee iliyokuwepo Makao Makuu ya Wilaya, Micheweni.
Umbali na ubovu wa barabara uliwafanya kinamama waone bora kujifungulia nyumbani na gari hizo zilipoharibika ndio ukawa mwisho wa huduma hiyo.
Mbunge huyo alisema, alitumia pesa za Jimbo kukwangua barabara za Kiyuyu, Chanjahani ili ziweze kupitika kwa urahisi kutokana na kuwa mbovu na zisizopitika.
Kwa kuwashirikisha wananchi walichimba visima vya maji Kiyuyu na Chanjahani ambavyo hata hivyo vilikauka na wakaendelea kubaki na shida ya maji.
Alisema, amepigia kelele suala hilo bungeni miaka kadhaa aliyokuwa katika kiti hicho lakini hakuna la maana lililofanyika.
Uvuvi haramu ilikuwa changamoto kubwa jimboni humo na mbaya zaidi wavuvi hao hawakuwa na vifaa vya kisasa zikiwemo boti.
Hali hiyo iliwafanya kushindwa kwenda mbali zaidi baharini kuvua na wakabaki maeneo jirani wakifanya uvuvi haramu.
Uvuvi na kilimo ndio zikawa njia pekee za vijana na kinamama kujiajiri hali ambayo iliwafanya wengi kukimbilia mijini na maeneo mengine kutafuta ajira na kutekeleza vijiji vyao vya asili.
Shule zilikuwa zinahesabika hivyo kuwafanya wanafunzi kutembea umbali mrefu hali ambayo iliwafanya wengine kukatiza masomo.
Kijiji cha Makangale chenye wakazi zaidi ya 5,000 hakikuwa na maji hivyo kuwafanya wakazi wa Kijiji hicho kila siku kuwa katika mihangaiko ya kutafuta maji.
Mbunge huyo alisema, miaka minne ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mbunge Mohamed Said Issa, barabara ni ya lami kutoka Konde hadi Micheweni.
Alisema, ana shule tatu za kisasa za ghorofa na hakuna tena mtoto anayetembea umbali mrefu kufuata shule, maji yapo takribani vijiji vyote.
Uwekezaji wa ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii umeshika kasi, bandari kavu na boti zilizotolewa kwa wavuvi kumeibadili Konde na vitongoji vyake.
Aliendelea kusema, hivi sasa wananchi wake wanafurahia huduma za msingi kuwa karibu chini ya mfumo wa elimu na huduma za afya bure ambao uliasisiwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Ajira zimefunguka na mamia ya vijana wanarudi na wasaka ajira wapya wameibuka jimboni humo.
Mbunge huyo ni mmoja kati ya wengine kadhaa wa ACT-Wazalendo na CCM, Unguja na Pemba ambao kero za wananchi wao zimetatuliwa.
Kutokana na mabadiliko hayo ni wazi kuwa wabunge na wawakilishi wa ACT Wazalendo wana kazi ya ziada kuwaaminisha wananchi wao kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), chini ya CCM haifai.
Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye hotuba zake mara kadhaa amekuwa akisisitiza kwa kusema, huo ni mwanzo na anataka apewe muda zaidi ili aifanye Zanzibar kuwa nchi ya mfano ulimwenguni.
Mmoja wa wabunge wa chama hicho pinzani ambaye hataki jina lake kutajwa hadharani alisema, kurejea kwao Bungeni au baraza la Wawakilishi, itategemea bahati zaidi kuliko ukweli.
“Jamaa katumaliza lakini no way lazima kubadilika kulingana na mazingira lakini kimsingi kero nyingi zimetatuliwa,” alisema.
Hata hivyo, alisema watapambana lakini pia kitendo cha karibuni cha baadhi ya viongozi wao wa wilaya na mikoa ya miwili ya Pemba kuhamia CCM kumewaacha njiapanda.
Mbunge huyo anamlaumu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Jussa Ismail Ladhu kwa kujali maslahi yake binafsi kuliko ya chama.
“Anakifanya chama hicho kama chake visiwani humo na huenda kikamfia kwani licha ya viongozi hao kuhamia CCM hajashtuka yupo Dar es Salaam,” alisema.
Makamu huyo anadaiwa kutoambilika na mwenye hasira anapokosolewa na hata anavyosema kuwa anaendeleza kazi aliyoiacha Maalim Seif Sharrif Hamad anajidanganya, kwani Maalim hakuwa mropokaji.
“Maalim Seif alikuwa mchambuzi, mwenye fikra pana ambaye hakuwa mtu wa kupayuka au kuzusha,” alisema na kuongeza kuwa, maendeleo yaliyopatikana hivi sasa yanawaweka njiapanda hivyo wasijue watapanda majukwaani na hoja gani.
Kulingana na vyanzo mbalimbali, Dkt. Mwinyi hadi hivi sasa ametimiza zaidi ya asilimia 90 ya ahadi zake na kwingineko ametekeleza hata yale ambayo akuahidi.
Kutokana na hali hiyo ni wazi kuelekea Oktoba 2025, huenda wabunge kadhaa na wawakiishi wakaunga mkono jitihada zinazofanyika sasa kama sio kuachana na siasa, wachambuzi wa masuala ya siasa, wanaamini kuwa kinachosubiriwa ni muda na sio vingine.