Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema madai ya Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Jussa Ismail Ladhu kuwa mchakato wa upatikanaji wa kampuni ya kuendesha bandari ya Zanzibar una walakini, hayana msingi wowote na hajui analosema.
Mbali na madai hayo, Jussa pia anadai kuongezeka kwa gharama za kutoa mizigo katika bandari Kavu zilizoanzishwa Fumba na Marhubi kipindi hiki cha Ramadhani na kusababisha kuwaongezea wananchi mzigo na ucheleweshaji wa makontena na meli kukaa muda mrefu bandarini.
Makamu Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo alidai ucheleweshaji huo, umechangia uhaba wa bidhaa za vyakula sokoni madai ambayo Katibu Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itiikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis ameyakanusha.
Alisema, Jussa sio mkweli au amedanganywa na jambo baya zaidi mengine anayajua, lakini hataki kusema ukweli, na badala yake anabaki kwenye propaganda na kuweka wazi kwamba, suala la gharama zaidi za kutolea makontena bandarini ni makubaliano baina ya mwenye mzigo na watoaji huduma binafsi, lakini bei halisi zinaeleweka kwa magari ya bandari yanayotoa huduma hiyo.
Mbeto alifafanua mchakato wa kuipata kampuni ya kutoa huduma bandarini Zanzibar ulipitia katika mchakato sahihi ikiwa ni pamoja na kushirikisha Mamlaka ya Bandari Zanzibar na vyombo husika ikiwa ni pamoja na timu ya majadiliano ya Serikali ya Mapinduzi (GNT).
Alisema, zabuni iliitishwa na kampuni zilizoomba anazitaja kuwa ni pamoja na African Global Logistics, Oman Investment Authority (OIA), DP World na Head Port ya Abu Dhabi na kampuni iliyoshinda zabuni ni African Global Logistics (AGL), ambayo ni Kampuni tanzu ya Midetereniani Shiping Company (MSC).
Alisema, kampuni hiyo ilibidi kuanzisha kampuni tanzu kwa mujibu wa sheria ambayo itaendesha bandari ya Malindi na ndipo ilipoundwa kampuni ya Zanzibar Mult Pulpose (ZMT) na AGL ni kampuni yenye uzoefu wa miaka 20 ikiwa inafanyakazi katika bandari zingine 15 barani Afrika.
Anazitaja baadhi ya bandari hizo na nchi zake kwenye mabano ni Dakar Terminal (Senegal), Conacry (Guinea), Freetown (Siera Leon), Lome (Togo). Monrovia (Liberia), Abdjan (Ivory Coasta), Lome (Togo)Point Nero (DR Congo). Lagos (Nigeria) na kwingineko.
Alisema, sio kweli kwamba kampuni hiyo haina uzoefu na hoja kuwa wamepewa umiliki wa asilimia 70 “Yeye alitaka wapewe ngapi? Wamezingatia vigezo vinavyotakiwa na ndio maana walikataa uwekezaji wa DP World ambao walitaka kutoa asilimia 5 na Abu dhabi waliotaka kutoa umiliki wa asilimia 3 kwa Zanzibar.
”Hao tuliwakatalia na tuliamua kukaribisha uwekezaji bandarini Zanzibar kufuatia malalamiko aliyopewa Rais Dkt. Mwinyi na wafanyabiashara kuwa mizigo yao inachelewa na hakuna ufanisi kiutendaji bandarini hapo” alisema.
Sharti jingine walilokataa la DP World ni kuwataka wasiendeleze bandari zingine ambazo walishaanza kufanya hivyo ambazo ni bandari ya Manga Pwani, Shumba na Wete jambo ambalo Mbeto alisema, kwa mtu mwenye akili hawezi kukubali na kufafanua kwamba, mkataba baina ya mwekezaji huyo na SMZ ni miaka mitano.
“Nilimsikia Jussa kuna kitu anakitaja kinaitwa Terminal Operation Systeam (TOS) hii sasa hivi hata DP World Dar es Salaam hawatumii mfumo huo wa gharama zote kuziweka pamoja, nao sasa wameiga mfumo wa Zanzibar,” alisema Mbeto.
Anabainisha kuwa, tozo zilizopo hadi sasa ni kwamba makontena ya futi 20 (114) na futi 40 dola (180), ISPS dola 25 kwa kontena zote na sio kama anavyosema yeye kuwa ni kwa kila kontena.
Alisema, MHC ni dola 45 kwa kontena zote na huduma za ubebaji na upangaji wa makontena bandarini ni dola 30 kwa kontena za ukubwa wote, H Over ni dola 70 zote na tozo hizo hazijabadilika na pia alizungumzia bandari kavu.
“Tozo inayotozwa na bandari ni dola 65 tu kwa gari linanalosimamiwa na bandari fedha ambazo ni sawa na Shilingi 150,000,” alisema na kuongeza kuwa Jussa anadai baadhi ya magari wanalipa 300,000; huo ni uamuzi wa mtu kwa mtoa huduma na kila mtu ana bei zake lakini sio bei elekezi.
Alisema, bei zinaeleweka na mtu anapotumia mtu binafsi kumsafirishia kontena la gari lake kwa bei tofauti na inayotozwa na magari ya bandari hiyo inakuwa ni makubaliano yake na watoaji si SMZ wala bandari wanaohusika.
Alisema, kwa kuwa mwezi wa Ramadhan una shughuli nyingi, hivyo Serikali ikaamua kuanzisha bandari kavu nyingine ili kurahisisha utoaji mizigo kipindi hiki na ndio maana wanatumia kwa muda eneo la Fumba ili kupunguza msongamano.
Bandari Kavu inatumika pia Marhubi kwa bidhaa ambazo zinahusiana na mwezi wa Ramadhani watatolea huko, na kuhusu uhaba wa bidhaa za vyakula hilo halina ukweli, kwani hivi karibuni wakati wa ziara ya Rais Dkt.Mwinyi masokoni suala hilo halikujitokeza. “Hakuna mfanyabiashara hata mmoja aliyelalamika kwa Rais kuwa kuna uhaba wa bidhaa za vyakula.”
Aidha, Mbeto alizungumzia suala la muda wa meli kukaa bandarini ambapo alisema, awali meli zilikuwa zinakaa siku 20 hadi 40, hivi sasa kushusha iwe meli kubwa au ndogo hazizidi siku mbili na haizidi siku tatu na wala hakuna gharama kuongezeka kwa kupeleka bidhaa bandari kavu.
Aliongeza: “Hata anaposema hakuna uwekezaji uliofanywa bandarini sio kweli, kuna vifaa vimeongezwa na awali Serikali kuna vifaa ilikuwa tayari imenunua kwa ajili ya maboresho ya bandari ikiwa ni pamoja na mashine tatu za kushushia makontena.”
Alisema, mtu aliyekamilisha taratibu zinazotakiwa katika kituo kimoja (One Stop Centre), hapati tabu kutoa mzigo wake iwe bandari kavu ya Marhubi au Fumba na alibainisha kuwa awali meli zinazoleta bidhaa za vyakula kama mchele, tende na zingine zilikuwa zinachelewa hadi siku 40 lakini sasa bidhaa hizo zinatolewa bandari kavu ya Fumba.
“Kama kuna kuchelewa kidogo ni katika mifumo ya TRA ambao wameweka mfumo mpya ambao hata hivyo kadiri siku zinavyokwenda unazidi kufanya vizuri,” alisema na kuongeza suala la kuchelewa meli nje ya bandari nalo limepotoshwa.
Alitoa mfano wa meli ya Laura aliyoitaja Jussa alisema, kukaa nje ya bandari haizidi siku nane na siku za ushushaji bandarini ni siku mbili hadi tatu kutegemea na ukubwa wa meli na jambo la ajabu Jussa kachanganya meli kubwa na ndogo na zote kwenye kushusha si zaidi ya siku tatu.
“Sasa huo urasimu anaoungumzia Jussa unatoka wapi? Kama sio uzushi,” alisema na kuongeza kuwa, hajui Jussa ana tatizo gani na hakuna kampuni ambayo ilipewa mkataba kisha akapewa mwingine na kuhusu maslahi ya wafanyakazi wa bandari.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi ambayo Jussa alifananisha bandari ya Zanzibar na Dar es Salaam, Mbeto alisema.”bandari ya Dar es Salaam haiwezi kufananishwa na Zanzibar kwa kuwa kule ni lango la nchi zingine sita wakati ya Zanzibar ni kwa ajili ya Zanzibar pekee, hivyo ni wazi kuwa meli zitakuwa nyingi na hata maslahi ya wafanyakazi hayawezi kufanana.”
Katika hatua nyingine, Mbeto alisema Mapato ya bandari yameongezeka maradufu baada ya uwekezaji wa sasa na yametoka Shilingi Bilioni 3.7 na sasa wanaelekea makusanyo ya Shilingi Bilioni 8 na analalamikia mawakala wasio waadilifu ambao hufanya udanganyifu kwa mizigo kuwa tofauti na iliyomo,
Alisema, Mawakala wasio waadilifu wamekuwa wakilazimisha kutokufanyika ukaguzi na hakuna mfanyabiashara anayelalamika na ratiba ya meli zinazoingia bandarini huwa haibadiliki na meli kubwa kadhaa zipo nje zinasubiri kuingia bandarini kushusha.
“Bandari inaendeshwa kwa faida na hakuna zabuni iliyotolewa na wala sio mwekezaji wa Mpendae ni wa Kimataifa, hivyo Jussa aache uzushi,” alisema na alimtaka mwanasiasa huyo akajiridhishe na hakuna upotevu wala Serikali inachopoteza.