‘Muungano wetu umedumu kutokana na dhamira za dhati…’

0

SERIKALI ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo hufadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa pande mbili za Muungano.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni wakati akifungua semina ya mafunzo ya Wabunge wa Zanzibar wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kuhusu mfuko wa jimbo na taasisi za Muungano iliyofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Zanzibar, Februari 28, 2025.

Alisema, miradi na programu hizo ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Miradi ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kutokana na kuongezeka kwa kina cha Bahari ya Hindi-Sipwese Pemba, Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi kwa Vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu (Mamlaka ya Elimu Tanzania – TEA) pamoja na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA).

“Mtakubaliana nami kuwa, Muungano wetu umedumu kutokana na dhamira za dhati za umoja walizokuwa nazo Waasisi wake, Sera makini za Serikali zote mbili za TANU na ASP na sasa CCM, jitihada zinazoendelezwa na viongozi waliofuatia baada ya Waasisi pamoja na kuungwa mkono na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mifumo imara iliyowekwa ya kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoukabili Muungano wetu, imewezesha pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano kupiga hatua kubwa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na hivyo kupata sifa kubwa Kimataifa,” alisema Waziri Masauni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here