Dkt.Samia awashukuru Muheza kwa kumchagua ‘Mwana FA’

0

RAIS wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa watu walikuwa na wasiwasi alipowateua Hamis Mwinjuma (Mwana FA) kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na Nickson Simon (Nikk wa Pili) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.

Hata hivyo, alisema viongozi hao wamethibitisha kuwa hatua ya kuwateua hakukosea kwa kuwa wamekuwa na msaada mkubwa katika Taifa.

Akizungumza leo Februari 27, 2025, wilayani Muheza, Mkoani Tanga, Rais Samia amesema: “Nawashukuru sana Muheza kwa kumlea kijana wetu Mwana FA, Hamisi Mwinjuma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Mbunge wenu. Kijana huyu anatusaidia sana Kitaifa,”

“Nilipomteua yeye na yule Mkuu wangu wa Wilaya ya Kibaha, Nikk wa Pili, watu hawakuelewa. Walisema huyu Mama anateua wachepe hawa, hawa wamezoea majukwaa na kurap, watakwenda kufanya kazi gani? Lakini kwa faraja na fahari kubwa, leo nataka kusema kuwa hawa wananisaidia sana,” alisema Dkt. Samia.

Rais Samia aliongeza kuwa, Hamis Mwinjuma, kama kijana na msanii, amepewa wizara inayohusika na vijana na wasanii, kwani yeye ndiye anayefahamu lugha ya kuongea na vijana na wasanii.

Alisema, kwa kiasi kikubwa, wizara hiyo chini ya mawaziri tofauti imekuza sana sekta ya sanaa na michezo, na hilo limetokana na uwepo wa watu wanaojua sekta hizo vizuri.

Hivyo, amewaomba wananchi wa Muheza kumlea Mwana FA na kumsaidia katika kazi yake ya ubunge.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Jitegemee wilayani Muheza, MwanaFA katika hotuba yake aliyoipa jina “Asante Mama”, alisema kuwa wilaya hiyo tangu ianzishwe haijawahi kupata miradi mingi kama kipindi cha uongozi wa Rais huyo.

Akizungumzia sekta ya afya alisema kuwa serikali ilimpatia kiasi cha Shilingi Bilioni 5.1 ambapo Shilingi Bilioni 4.3 zilienda katika hospital ya Dkt Samia Suluhu Hassan lakini pia walipewa Shilingi Mlioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya Kwafungo.

Alisema, walimalizia ujenzi wa zahanati Saba na Sasa tayari Serikali imeaahidi kumpatia pesa kiasi cha Shilingi Milioni 649 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kitakachojengwa Kijiji cha Mgambo kilichopo kata ya Misalai tarafa ya Amani.

Kwa upande wa elimu, alisema katika kipindi cha miaka minne wameweza kujenga vyumba 219 vya shule ya msingi na vyumba 106 vya sekondari tofauti na utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambapo walijenga vyumba 20 tu vya madarasa.

Hata hivyo, alimwambia Rais kwamba katika kuunga mkono juhudi zake yeye (FA) na marafiki zake wamejenga shule ya msingi katika Kijiji cha Misufini kilichopo kata ya Magoroto baada ya kuona namna watoto wanavyopata shida ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.

Aliwataja marafiki wake kuwa ni Rasheed Karimjee aliyejenga vyumba viwili na benki ya CRDB tawi la Muheza ambalo limejenga vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo.

Kuhusu Umeme alisema, vijiji vyote vimepata Umeme na vitongoji 45 bado havijapata huduma hiyo, lakini kati ya hivyo vitongoji 30 vimeingizwa kwenye mpango wa REA na vingine 10 hivyo vitabaki vitatu ambavyo mbunge alimshukuru Rais kwa kusema kuwa “kabla ya uchaguzi vitapata Nishati hiyo.”.

Aidha, kuhusu maji alisema wakati alipoanza kulitumikia jimbo hilo, upatikanaji wa Maji mjini ilikuwa ni asilimia 41 na Vijijini ni asilimia 43 ambapo kwa miaka hii minne upatikanaji huo umekuwa asilimia 71 mjini na Vijijini ni asilimia 73.

Mbunge huyo alisema, utakapokamilika mradi wa Maji wa miji 28 wilaya ya Muheza upatikanaji wa Maji itakuwa ni asilimia 100 kupitia mradi huo.

Alisema, pamoja na mafanikio hayo, kuna changamoto za wakulima wa machungwa kukosa soko la uhakika kiasi kwamba madalali wamekuwa wakiwanunuza wakulima mashambani na kuwafanya wasipate maendeleo.

Akamuomba Rais, Serikali iwapatie soko la Kimataifa pamoja na lile la viungo, ambapo katika wilaya hiyo imekuwa ikizalisha kwa wingi.

Suala jingine ni kupatikana kwa mashine ya korona katika shamba la kibaranga, ambako wakulima wadogo wamekuwa wakipata shida kuchakata mkonge wao.

Pia, alimuomba Rais kuwasaidia fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Muheza – Amani Kilomita 38, ambapo wakati anaingia madarakani kulikuwa na Kilomita Saba zilitolewa na Serikali, lakini mkandarasi hajalipwa, hivyo alifuatilia akalipwa kisha akapewa tena Kilomita Saba na Sasa amepewa Kilomita nne.

Akijibu maombi ya mbunge huyo, Rais Samia alisema, suala la barabara zitawekwa lami pamoja na ile ya Muheza kwenda Pangani ambayo itaingizwa kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 ikiwemo kujengwa shule za sekondari katika kata mbili ambazo hazina sekondari.

Vile vile, Rais Samia alisema Serikali itaharakisha ujenzi wa soko la machungwa na akaitaka Wizara ya viwanda kuharakisha kutafuta wawekezaji ili kumaliza tatizo hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here