Na Mwandishi Maalum, Pemba
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimevunja mwiko wa kisiasa kudhani Pemba ni mateka wa upinzani na kwamba wanaweza kufanya watakavyo kwa kuendesha siasa za kufikirika.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo kufuatia wanachama zaidi ya 2500 kukihama ACT Wazalendo na kujiunga CCM .
Mbeto alisema, tokea mwaka 1995, upinzani umekuwa ukiifanya Pemba ni kichaka cha kufanya siasa za uongo, kupotosha dunia na kukigeuza kisiwa hicho, shamba la mapato binafsi ya wanasiasa wao wanaotajirisha.
Alisema, kwa muda mrefu Pemba imetumika kubadili maisha binafsi ya wanasiasa wa upinzani wanaochaguliwa Udiwani, Ubunge na Uwakilishi huku wawakilishi hao wakishindwa kutatua changamoto za wananchi.
“CCM kimevunja mwiko wa kuifanya Pemba mateka wa upinzani. Kuna baadhi ya wanasiasa walidhani wangeifanya Pemba watakavyo. Wamewatumia sana wananchi ili kufikia matlaba yao. Zama hiyo sasa imepita,” alisema Mbeto.
Aidha, aliongeza kuwa utendaji wa Serikali ya awamu ya Nane Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imewafumbua macho wananchi wa Unguja na Pemba sasa wanafurahia mwamko wa maendeleo.
“Zama ya siasa za kuwagawa wananchi kwa Upemba na Uunguja imepitwa na wakati. Wazanzibari wanajitambua ni wamoja na hawatogawanyika au kudanganyika,” alisema Mbeto.
Pia, Katibu Mwenezi huyo alisema, mabadiliko ya miaka minne ya maendeleo toka Rais Dkt. Mwinyi awe madarakani, uongozi wake umeleta mabadiliko makubwa ya maendeleo yanayoonekana Unguja na Pemba.
“Miaka mitano ijayo Rais Dkt.Mwinyi ataifanya Zanzibar kuwa nchi inayotamaniwa na kila binadamu kuishi. Maendeleo yake yataishangaza dunia na kuwa kimbilio la kila mtu; aidha kutamani kuishi, kuwekeza miradi au kutalii,” alisisitiza Mbeto.