CCM: Wananchi Pemba jitokezeni kujiandikisha

0

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM ) kimewataka wananchi wote Kisiwani Pemba ambao bado hawajajiandiikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga kura, wajitokeze kutumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia .

Wito huo umetokewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alipotembelea Kisiwapanza Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

Mbeto alisema, lazima wananachi wote wenye sifa ya Ukaazi kwa mujibu wa sheria, wajitokeze ili kujiandikisha kuwa wapiga kura halali watakaowachagua viongozi ifikapo Oktoba mwaka huu.

“Zoezi la uandikishaji hadi sasa linakwenda vyema hakuna rabsha zozote. Kila mtu akitii sheria na kufuata taratibu mambo yatakwenda kwa murua . Ni haki ya kila mwananchi Mkaazi kuandikishwa,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisisitiza kuwa wakaazi wote ambao majina yao hayamo kwenye Daftari la Ukaazi kwa Sheha mhusika ndio ambao hawatapata nafasi ya kuoredheshwa kwa mujibu wa sheria.

“Wananchi ndio wapiga kura wanaoziweka serikali madarakani. Kila mwenye haki ya kupiga kura atapewa nafasi ya kuandikishwa na kuwa mpiga kura halali,” alisisitiza.

Hata hivyo, Mbeto aliendelea kusisitiza na kuwataka wanasiasa wenzake kuwa na tahadhari ya matamshi yenye kutia shaka ambayo yanaweza kuleta sintofahamu wakati kila kitu kinakwenda vizuri hadi sasa.

Mbeto ameshatembelea majimbo manne ya Mkoa kusini pemba katika vituo vya Muwambe, Shamiani, Makoongwe na Kisiwapanza akiwahimiza wananchi kujitokeza na kujiandikisha.

“Demokrasia ya uchaguzi isiwe chanzo cha kuipotezea amani nchi yetu pendwa. Kila mwanasiasa lazima ajenge uvumilivu, awe msema mkweli, asiwe mchochezi na kuwa chanzo cha kuvuruga amani,” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here