RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameizawadia Timu ya Taifa ya Zanzibar ‘ZANZIBAR HEROES’ Shilingi Milioni 50 baada ya kulitwaa Kombe la Mapinduzi 2025.
Akizungumza katika Hafla Maalum ya Chakula cha Mchana aliyoiandaa kwa ajili ya Wachezaji wa Timu hiyo katika Viwanja Vya Ikulu, Rais Dkt.Mwinyi ameeeleza kuwa, timu hiyo imeiletea heshima kubwa Zanzibar na Kudhihirisha kuwa kuna Vipaji vingi vya Soka hapa nchini vinavyopaswa kuendelezwa katika Maeneo mbalimbali..
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa, kwa mafanikio ya ‘Zanzibar Heroes’ kuna kila sababu kwa Serikali kuendelea na ujenzi wa Academy za Soka Kila Mkoa kwa lengo la kuviibua Vipaji vya Vijana.
Rais Dkt.Mwinyi ametangaza Dhamira ya Kuunda Kamati Maalum ya Kitaifa hivi karibuni itakayokuwa na Jukumu la Kumshauri namna bora ya kuuendeleza Mpira wa Miguu hapa nchini.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa hatua za Timu za Zanzibar kulibakisha Kombe la Mapinduzi kwa Mwaka wa Tatu mfululizo kunaashiria uwezo mkubwa wa Soka na Vipaji viliopo .
Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa, Tayari Wagunduzi wa Vipaji vya Soka (SCOUT) wa Nchini Uturuki wameonesha nia ya kuja Zanzibar baada ya Kuushuhudia Mchezo wa Fainali baina ya Zanzibar na Burkinafaso na kukiri Kuwepo Vipaji Vingi.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa lengo ni kuwa na Timu imara za Mpira wa Miguu katika ngazi zote zitakazoiletea heshima Zanzibar.