THBUB yachunguza mauaji ya watu wawili Pemba

0

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema inachunguza vifo vya watu wawili vilivyotokea hivi karibuni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.


THBUB imeeleza imepokea kwa masikitiko makubwa vifo vya Athuman Hamad Athuman na Amour Khamis Salim, waliokuwa wakaazi wa kijiji cha Kiungoni, Wete, Pemba vilivyotokea mwezi Disemba mwaka 2024.


Akitoa tamko la Tume hiyo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, ofisini kwake Mbweni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna wa Tume hiyo Zanzibar, Khatib M. Mwinchande alisema, tukio la mauaji hayo ni ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 13(2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinachoeleza kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwenye jamii kwa mujibu wa sheria, hivyo Tume imelaani vikali vitendo hivyo.


Kamishna Mwinchande amebainisha kuwa,, mauaji hayo ya Kiungoni Pemba yametokea wakati THBUB inaendelea na kazi ya kufuatilia mauaji ya Kidoti, Kaskazini Unguja na matukio mengine kama hayo kwa upande wa Tanzania bara ambayo yanarudisha nyuma juhudi za Serikali zetu mbili za SMZ na SMT za kuimarisha ulinzi, amani na usalama wa raia na mali zao nchini.


Aidha, Kamishna Mwinchande alisema, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilidai kwamba wakati wa uhai wao, marehemu walichukuliwa na askari wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya wakiwa wazima kwa tuhuma za kuhusishwa na wizi wa baskeli na matumizi ya bangi, lakini walirejeshwa siku ya pili wakiwa wamefariki.


Amebainisha kuwa, mauaji hayo ni Ukatili dhidi ya binaadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 13(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Pia alieleza kuwa mauaji hayo ni Ukiukwaji wa haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru kama ilivyotamkwa kwenye Ibara ya 15(1)(2) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Akizungumzia suala la Utawala Bora, Kamishna Mwinchande alisema, mauaji hayo ni Ukiukwaji wa Msingi wa Utawala Bora hususan utawala wa Sheria.


Aidha, ameeleza dhamira ya THBUB ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuendeleza uchunguzi kwa matukio mengine kama hayo, ni kulinda misingi ya utawala Bora na Utawala wa Sheria nchini.


Halikadhalika, Kamishna Mwinchande ametoa wito kwa wananchi na jamii, kutoa ushirikiano kwa THBUB na vyombo vyengine vya uchunguzi vinavyochunguza tukio hilo.


Vilevile ameeleza, THBUB inawakumbusha wananchi na taasisi zote, umuhimu wa kupiga vita vitendo vyote vinavyokiuka Sheria, ukiukwaji wa misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu, kwa kuwa haki ya kuishi ni haki ya msingi kwa kila mtu.


Kwa upande mwengine ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Athuman Hamad Athuman na Amour Khamis Salim kwa msiba mzito wa kuondokewa na wapendwa wao kwa njia hiyo, pamoja na kuwaomba wananchi kuwa watulivu na wenye subira hususan wakati huu ambao vyombo husika vinaendelea na uchunguzi wa matukio ya mauaji.


Marehemu Athuman Hamad Athuman alifariki dunia akiwa na miaka 75 na Amour Khamis Salim alikufa akiwa na miaka 28 wote walikuwa wakaazi wa Kimango Kiungoni, Wete Pemba. Waliodaiwa kukamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupamba na dawa za Kulevya Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here