RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imevuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 ilioainisha Ujenzi wa Kilomita 275 za barabara.
Ameeleza kuwa Serikali imeamua kuongeza idadi ya barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami hadi kufikia Kilomita 300 Mijini na Vijijini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipoifungua Barabara ya Ukutini -Bandarini Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, Januari 10, 2025.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alisema Mkataba wa Wananchi na Serikali yao ni Ilani ya Uchaguzi hivyo kuna kila sababu ya kujivunia kwa yote yaliofanyika Katika Ujenzi wa Barabara.
Akizungumzia barabara ya Ukutini -Mtangani Bandarini alioifungua alisema ni hatua muhimu ya kufungua fursa za Kiuchumi.
Ameeleza kuwa mbali na Usafiri barabara hiyo ya Ukutini – Bandarini itafungua Fursa za Ajira kwa kuwa kuna Bandari na Hoteli katika eneo hilo pamoja kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijami ikiwemo Hospitali, Skuli na Usafirishaji.
Ufunguzi wa Barabara hiyo kunakamilisha Idadi ya Kilomita 85.5 za Barabara zilizojengwa katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Barabara ya Ukutani – Bandarini yenye Kilomita 4.6 iliojengwa na Kampuni ya IRIS kugharimu Dola Millioni 2.658 ni miongoni mwa Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Ndani zenye Urefu wa Kilomita 275 .9.