Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema hadi kufika mwishoni mwa mwaka huu 2025, Zanzibar itakuwa na mabasi na treni za umeme na teksi za kwenye maji ikiwa ni sehemu ya usafiri wa umma wa kisasa mjini tofauti na ilivyo sasa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo cha mabasi cha Kijangwani hivi karibuni, Rais Dkt.Mwinyi alisema huku akijibu tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kuhusu ufisadi na ongezeko la deni la Taifa.
Bila kumtaja, Rais Dkt. Mwinyi alisema hivi sasa kuna mpango mpya wa usafiri wa kisasa wa umma katika mji wa Zanzibar baada ya kukaa na kuona umuhimu wa aina hiyo ya usafiri na kuondokana na magari ya shamba (Chai Maharage), kuja mjini.
“Wakati tunaadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi, hatuwezi kuendelea kutumia magari ya shamba kuja mjini, ipo sababu ya magari yale kuitwa ya shamba, yanakuwaje mjini?” alihoji na kuongeza kuwa, huwezi kwenda nchi yoyote Duniani ukakuta Chai Maharage zipo katikati ya Jiji, hivyo Zanzibar imeazimia kutakuwa na mabasi ya umeme ya kisasa.
Alisema, anaposema Zanzibar kutakuwa na mabasi ya umeme, treni na teksi za kwenye maji wanafikiri anatania, lakini alibainisha kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu, Unguja kutakuwa na mabasi ya umeme, ndio maana vinatakiwa vituo vya kisasa viendane na mabasi wanayozungumzia.
Licha ya Kijangwani vituo vingine kama hivyo, vitajengwa Jumbi, Mwanakwerekwe na Mwera na mtu akitaka kwenda mikoa yote Unguja, atatumia usafiri huo na ndani ya Mji vitajitajika vituo vingine vya ziada ambavyo alisema vitakuwa Kijangwani, Malindi, Hospitali ya Mnazi Mmoja na Michenzani.
Alisema, licha ya maendeleo yanayofanyika wapo watu wanataka kumkatisha tamaa kwa kusema maneno ya uongo na uzandiki na hatayumbishwa kwani Serikali inakopa kwa nia njema ya kujenga miradi ya maendeleo na alishangaa wanaozungumzia madeni mbona wapo kimya kuhusiana na Akaunti Maalum ya Kulipa Madeni?.
Rais Dkt. Mwinyi alisema ongezeko la deni la Taifa toka waingine madarakani ni asilimia 50 na sio 208 kama inavyoelezwa kwani awali deni lilikuwa Sh800 bilioni baada ya miaka minne hadi sasa limepanda hadi Sh1.2 Trilioni sawa na ongezeko hilo la asilimia 50.
“Lakini imesemwa kila Mzanzibari kwa sasa amebebeshwa deni la Shilingi 119,000” alisema na kuongeza kuwa, lengo lao hao wanaoeleza hivyo, lengo “ionekane tudaiwa lakini wanaposema hivyo ndani ya akaunti ya madeni tuna Dola za Marekani 250 Milioni.”
Fedha hizo, sawa na karibu Shilingi 600 Bilioni na kuwa na kiasi hicho maana yake deni linahimilika, hivyo wanaweza kukopa tena, kwani uwezo wa kuzipata hizo Shilingi 600 Bilioni ni miezi miwili na kama makusanyo ni Shilingi 300 Milioni kwa mwezi hakuna sababu ya kuogopa kukopa.
Alisema, hata Mataifa makubwa ya Marekani, Uingereza na Ufaransa wanakopa na ndio wenye madeni makubwa. “Lazima ukope ili mradi uwe na uwezo wa kulipa”
Katika hotuba yake wakati akitangaza nia ya kuwania Urais wa Zanzibar 2025 mbele ya waandishi wa habari Januari Mosi mwaka huu, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman Zanzibar, alidai kuwa nchi ina madeni ambayo haiwezi kuyalipa.
Alidai, kuna madeni makubwa ambayo wakopeshaji wa Kimataifa na nchi haina uwezo wa kuyalipa na akaenda mbali zaidi kuwa, kila Mzanzibari anadaiwa Shilingi 119,850 na wakopeshaji wa Kimataifa.
Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo alidai kuwa bado hatuwezi kuonyesha fedha hizo zilitumika kwa ajili gani, tuhuma ambazo Dkt.Mwinyi alisema hazitoweza kumyumbisha katika kuwaletea watu wake maendeleo na aliziita ni maneno ya uongozo na uzandiki.
Dkt.Mwinyi alikemea urasimu katika taasisi za serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo huo wa stendi ya kisasa ya mabasi Kijangwani na ameagiza yeyote anayekutana na urasimu kwenye utekelezaji wa miradi aende kwake moja kwa moja kumpa taarifa.
“Hatuwezi kukaa mwaka mmoja miwili tunazungumzia jambo moja, hatuna muda huo, tuzungumze wiki moja mambo yafanyike” alisema na awali Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya alikanusha kauli za wanasiasa wanaodai Mfuko wa ZSSF hauna fedha za kuwalipa wastaafu.
“ZSSF ina uwezo wa kuwalipa wastaafu kwa miaka 25 ijayo bila kufanya uwekezaji wowote” alisema na kubainisha kuwa wanaodai hivyo hawajui kuwa mikopo inayochukuliwa ndiyo inajenga na uwekezaji zaidi ndio thamani ya nchi inakua na toka 2000 hadi sasa thamani ya nchi imeongezeka maradufu.