Biashara kati ya Tanzania na China yafikia Dola Bilioni 8.78

0

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema, uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China umeendelea kukua ambapo mwaka 2023 biashara kati ya nchi hizo ilifikia Dola Bilioni 8.78.

Alisema, ukuaji na ushirikiano huo wa makampuni ya China na wafanyabiashara wa Tanzania umeleta maendeleo katika ukuaji wa viwanda vya ndani, kutengeneza ajira, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa hali ya maisha ya Watanzania.

Majaliwa alisema hayo leo (Novemba 30, 2024) wakati wa hafla ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Jumuiya ya Kukuza Ushirikiano kati ya China na Tanzania, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam.

Alisema, Kampuni za China zimezindua takribani miradi 1,274 ambayo kwa kiasi kikubwa pamoja na mambo mengine, imezalisha ajira kwa Watanzania. “Huu ni uthibitisho wa jinsi ushirikiano wetu unavyolenga kutoa fursa kwa wananchi wetu”.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa China katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, miundombinu na utamaduni”

Aidha, alisema China ni moja ya mshirika mkubwa wa kibiashara na uwekezaji kwa Tanzania na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo kwenye sekta za kilimo, madini, viwanda na maendeleo ya miundombinu.

Aliongeza, China imekuwa mshirika muhimu katika kuisaidia Tanzania kukabiliana na majanga ya kiafya ikiwemo magonjwa ya kuambukiza na changamoto za afya ya mama na mtoto. “China imekuwa ikitoa timu za wataalam, kuchangia vifaa, na kusaidia kujenga miundombinu ya afya. Ushirikiano huu umeokoa maisha ya wengi na umehakikisha kwamba watu wetu wanapata huduma bora za matibabu”

Akizungumza kuhusu Jumuiya ya Kukuza Urafiki kati ya Tanzania na China, Majaliwa alisema jumuiya hiyo imekuwa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ikiwemo kuwaleta watu pamoja, si tu kutoka kwa Serikali, bali kutoka nyanja mbalimbali za maisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here