‘Jenerali Musuguri ameacha alama ya uzalendo’

0

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano pamoja na kuifundisha jamii moyo wa dhati wa kuilinda nchi.

Dkt. Biteko alisema hayo Novemba 4, 2024 Butiama mkoani Mara wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Jenerali Mstaafu Musuguri.

“Katika uhai wa kila mmoja wetu ni jambo gani mtu atakumbukwa nalo, baba huyu ameacha alama ya uzalendo, kujitoa kwake na kuipenda nchi pia aligeuza changamoto kuwa fursa. Musuguri alikuwa mstari wa mbele kuliokoa Taifa lake, tujiulize sisi tuliobaki tutaacha alama gani? Yeye aliacha ya kulikomboa Taifa letu,” alisema Dkt. Biteko.

“Alikuwa kiongozi aliyetamani amani na alisisitiza hakuna vita iliyo nzuri aliamini nguvu ya mshikamano na katika kipindi hiki tunachoelekea cha uchaguzi tushikamane, tushirikiane na kuendelea kufanya amani iwe tunu ya Taifa letu,” alisisitiza Dkt. Biteko.

Fauka ya hayo, alisema Serikali itauenzi mchango wake daima na kutaja baadhi ya heshima alizowahi kupewa ikiwa ni pamoja na kutunukiwa medali mbalimbali mfano ya Vita ya Kagera na kuwa Serikali itaendelea kusimamia ujasiri, uzalendo na kuthamini amani.

Vilevile, ameihimiza familia ya Jenerali Mstaafu Musuguri kurithisha vizazi vyao mema yake pamoja na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao sambamba na kuwashukuru madaktari wote waliomtibu wakati akiugua.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax wakati akimkaribisha Dkt. Biteko kuzungumza alisema, Taifa limepoteza hazina na kamwe Jenerali Musuguri hatasahaulika kwa mema yake yote na kuwa Jeshi litaenzi mchango wake.

Naye, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda alisema, kifo cha Jenerali Musuguri ni msiba mkubwa si tu kwa Jeshi bali kwa Tanzania yote kulingana na mchango wake wa ulinzi alioutoa katika utumishi wa umma kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

“Alishiriki Vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilimjenga, kumkomaza na kumpa uzoefu mkubwa ambao aliporejea nchini alitumia kwa ajili ya kujenga nchi yake na kuandaa mipango mbalimbali ya kivita ambayo nchi yetu ilishiriki ikiwa ni pamoja na vita vya mvamizi Iddi Amini na vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.” alisema Jenerali Mkunda.

Akihubiri wakati wa misa hiyo ya mazishi, Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Musoma, Michael Msonganzila alisema, makundi mbalimbali ya watu yamekusanyika eneo hilo kwa ajili ya kumuaga Jenerali Mstaafu Musuguri na kuwa wameunganishwa na Jenerali huyo katika tukio hilo.

“ Kilichotukutanisha ni misa ya kumuombea Musuguri aende kwa safari ya amani kuelekea huko kwa aliyetuumba na alituumba tumjue, tumpende na tumtumikie na mwishowe twende kwake mbinguni” alisema Askofu Msonganzila.

Aliendelea kusema “ Kumuombea Jenerali huyu ni tendo la kiimani, tunaamini Yesu alikufa, akazikwa na kufufuka na pia tunaamini Mungu atawakutanisha wote waliokwisha fariki na Yesu Kristo”

Askofu Msonganzila amebainisha kuwa, mkusanyiko mkubwa wa watu unafanya watu watafakari kwa kina juu ya uhai wake na kuwa Jenerali Musuguri alikuwa mnyenyekevu, shupavu na kuwa alipigana vita vya haki wakati ambao Nduli Iddi Amin kutoka Uganda alivamia Tanzania mwaka 1978.

Kiongozi Mkuu wa Kabila la Zanaki, Chifu Japheti Wanzagi amesema kuwa Jenerali Musuguri alikuwa na sifa kadhaa ikiwemo unyenyekevu na mtu wa aina ya pekee ambaye alimjali na kumthamini na kusaidia kila mtu.

“Mzee huyu hakuwa na ukwasi wa mali bali utajiri wa utu wema, wengi wetu tulipenda kukaa nae na kuzungumza nae mara kwa mara. Kwa ujumla tunamshukuru Mzee kwa ukarimu na moyo wake wa kusaidia wahitaji,” alisema Chifu Wanzagi.

Jenerali mstaafu David Bugozi Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920 kijijini kwake Butiama na kufariki Oktoba 29, 2024 katika hospitali ya rufaa Bugando iliyopo Mwanza.

Alitumikia Jeshi kwa miaka 43 ambapo alihitimu kozi mbalimbali za Jeshi na kuwa Jenerali mwaka 1985.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here