Serikali yaendelea na uhakiki na ulipaji wa madeni ya wazabuni

0

Asia Singano na Peter Haule, WF

SERIKALI imesema, inaendelea na utaratibu wa ulipaji wa madeni mbalimbali ikiwemo madeni ya wazabuni wa chakula waliotoa huduma katika shule mbalimbali kwa kuzingatia upatikanaji wa mapato baada ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG) kufanya uhakiki wa madeni husika.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Jacob Tarimo, aliyetaka kujua mpango wa kuwalipa Wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali hususani chakula kwenye Shule za Serikali ambao wanadai kwa muda mrefu.

Chande alisema, lengo la Serikali kufanya uhakiki ni kutekeleza azma ya usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kulingana na sheria ya Bajeti SURA 439 na Sheria ya Fedha za umma SURA 348.

‘‘Wizara ya Fedha inazielekeza Halmashauri zote nchini kulipia huduma mbalimbali wanazopokea kutoka kwa watoa huduma kwa wakati ili kuepuka ulimbikizaji wa madeni na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa watoa huduma,’’ alifafanua Chande.

Kwa upande mwingine akijibu swali la Mbunge wa Chonga, Salum Mohammed Shaafi, aliyetaka kujua iwapo Akaunti ya Pamoja ya Muungano imeshafunguliwa, Chande alisema Serikali mbili zinaendelea na mashauriano juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu utaratibu wa kudumu wa Kuchangia Matumizi na Kugawana Mapato ya Muungano.

Aliongeza, uamuzi wa pamoja utakapofikiwa na pande mbili za Muungano, ndiyo utakaowezesha kufunguliwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here