TMDA yatoa ufafanuzi wa dawa inayodaiwa kubabua ngozi

0
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo

Na Andrew Chale

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)iliyo chini ya Wizara ya Afya, imetoa taarifa kwa Umma ufafanuzi kuhusu uvumi juu ya Dawa ya Paracetamol inayodaiwa kubabua ngozi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa Umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo imebainisha kuwa, imebaini uwepo wa taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa dawa aina ya Paracetamol ambayo imeandikwa P 500.

Akinukuu taarifa hiyo inayosambaa mitandaoni alisema:”Dawa hiyo inadaiwa kuwa ni paracetamol mpya nyeupe sana na inayong’aa, madaktari wanashauri kuwa ina virusi vya “Machupo”, inayochukuliwa kuwa moja ya virusi
hatari zaidi ulimwenguni, na kiwango cha juu cha vifo.”

Aidha, Mtoa taarifa anaitaka jamii kuisambaza kwa kila mtu aliyeko katika orodha yake ya mawasiliano ili kuokoa maisha. Anamalizia kwa kusema “Nimefanya sehemu yangu, sasa ni zamu yako. Kumbuka kwamba Mungu huwasaidia wale wanaosaidia wengine. Sambaza kama ilivyopokelewa’’.

Akielezea kuhusu taarifa hiyo, Dkt.Fimbo alisema, imekuwa ikijirudia mara kwa mara na TMDA imekuwa ikitolea ufafanuzi ikiwemo taarifa ya mnamo Mei 10, 2023, juu ya dawa aina ya P-500® (PARACETAMOL) ya Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India iliyodaiwa kuwa na virusi hivyo.

“TMDA inapenda kuufahamisha Umma kwa mara nyingine kwamba, hakuna virusi vinavyojulikana kwa jina la Machupo. Aidha, virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge.

Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa nahivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa.

Katika hatua hiyo, TMDA inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda afya ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.

Vilevile, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwenye Jamii.

TMDA yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa tiba nchini ambapo Ili kuhakikisha kuwa bidhaa tiba (zikiwemo dawa) zilizoko katika soko nchini zinakidhi matakwa ya usalama, ubora na ufanisi, TMDA imeweka mifumo mbalimbaliya udhibiti ikiwa ni pamoja na tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara
na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko.

Aidha, Wananchi wanaweza kupiga simu ya bila malipo: 0800110084 endapo wapatapo taarifa za mashaka kama hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here