Na Mwandishi Wetu
TANZANIA na Estonia zimekubaliana kushirikiana kufikia mapinduzi ya kidigitali duniani.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa kikao maalumu nje ya Kongamano la Kumi la Utawala wa Masuala ya Mtandao lililofanyika kwa siku mbili katika Jiji la Tartu nchini Estonia hivi karibuni.
Kongamano hilo lilishirikisha zaidi ya watu 500 kutoka nchi 67 duniani, wengi wakiwa watoa maamuzi ya maendeleo ya mambo ya kidijitali duniani, watunga sera, waratibu wa utekelezaji sera na wadau wa maendeleo.
Naibu Waziri Mahundi yeye na Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Nele Leosk ambaye ni Balozi wa Masuala ya Kidigitali wa nchi hiyo katika mkutano huo, kwa niaba ya nchi zao walizungumzia umuhimu wa kushirikiana katika uendelezaji na ukuaji wa akili mnemba, teknolojia ya mifumo kuzungumza na usalama wa mitandao.
Aidha, walizungumzia masuala ya namba ya utambulisho ya kidijitali, uhuru wa data, ukuzaji kampuni za ubunifu na uchumi wa kidigitali.
Katika mkutano huo mbali ya Naibu Waziri, wawakilishi wengine wa Tanzania walikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Uswisi, Joyce Malipula. Kwa upande wa Estonia, alikuwepo pia Mali Liis Vahi, Kansela wa Idara ya Mambo ya Kidijitali na Diplomasia ya Kimtamdao.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Maryprisca alishiriki pia katika Kongamano la Mawaziri wa nchi mbalimbali waliodhamiria kujenga uchumi imara wa Kidigitali.
Katika mkutano huo Naibu Waziri Maryprisca asisitiza nia ya Tanzania kuusuka uchumi wa kigiditali kwa kuhakikisha inaimarisha mifumo ukiwemo wa taarifa binafsi kwa wananchi wa Tanzania.
Mbali ya Tanzania, mawaziri wengine walioshiriki ni Mariin Ratnik, Waziri mdogo wa Mambo ya Maendeleo na Uchumi wa Estonia, Margus Tsahkna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Olalunbosun Tijani, Waziri wa Mawasiliano Ubunifu na Uchumi wa Kidijitali wa Nigeria na Mercy Wanjau, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kenya.