Vipaumbele 13 vya mageuzi elimu ya msingi na sekondari 2024/25

0

OR-TAMISEMI

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka 2024/25 imepanga kutumia Shilingi Trilioni 1.02 ili kutekeleza vipaumbele 13 kwenye sekta ya elimu vinavyolenga kusimamia na kuendesha Elimumsingi na Sekondari.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka huo, Waziri wa Nchi, TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema fedha hizo zitajenga vyumba vya madarasa 6,357, matundu ya vyoo 1,482, umaliziaji wa mabwalo 362 kati ya mabwalo hayo 15 ni msingi na 347 ni ya sekondari na umaliziaji mabweni 36 kwenye shule za awali na msingi.

Pia, alisema shule mpya 184, nyumba za walimu 184 na mabweni 186 katika shule za sekondari yatajengwa, sambamba na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwenye shule za awali 3, msingi 400 na shule za sekondari 500, ununuzi wa kemikali za maabara katika shule mpya 234.

Mchengerwa alisema, fedha hizo zitatumika katika utoaji wa ruzuku ya Elimu Bila Ada kwa shule za msingi 17,986 na sekondari 4,894;Ununuzi na usambazaji wa vitabu 2,215,877 kwa shule za msingi na 11,880,828 kwa shule za sekondari pamoja na vitabu na vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzia elimu ya awali kwenye shule 4,500.

Kadhalika, alisema wamepanga ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari; Kutoa mafunzo ya maadili kwa wakuu wa shule 17,220, viongozi na watumishi wa TSC 460 katika ngazi ya wizara na wilaya;Kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwenye shule za awali na msingi kwenye halmashauri 140.

Hata hivyo, alisema watatekeleza mpango wa shule salama kwenye shule za awali na msingi 2,500; Kuanzisha madarasa janja (smart classes) 10 kwa ajili ya ufundishaji mubashara katika halmashauri 10, kuandaa mwongozo wa mafunzo elekezi kwa walimu wapya wanaoajiriwa katika shule za umma na uandaaji wa kihunzi cha walimu wanaojitolea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here