AFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) Adam Mihayo amesema, wanataka kufanya uwekezaji mkubwa kwenye upande wa Kidijitali ili kurahisisha huduma kwa wateja wao.
Mihayo alisema hayo kwenye Mkutano na wahariri na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina, wenye lengo la kuelezea mafanikio ya benki hiyo ambayo inatarajia kutimiza miaka 100.
Alisema, uwekezaji huo utaifanya benki hiyo kuondokana na mifumo ya kizamani na hivyo kusaidia kusogeza huduma karibu na watanzania popote walipo, pia utaongeza wigo wa kuiongezea benki kipato sambamba na kushusha gharama za huduma zinazotolewa na TCB.
“Kufanya uwekezaji wa Kidijitali utasaidia kuondokana na mifumo inayofanya huduma kuchukua muda mrefu na kwa gharama kubwa zaidi, tunaamini kwa kufanya hivyo baada ya miaka mitano, tutakua zaidi na kushika namba tatu na hilo linawezekana,” alisisitiza Mihayo.
Alisema, kwa upande huo huo wa huduma za Kidijitali, hivi sasa wana mawakala zaidi ya 6,000 kutoka mawakala 1,500 ambao walikuwepo miaka mitatu iliyopita.
“Kwa hiyo tupo kila sehemu ya nchi, ingawa tunataka kuongeza mawakala zaidi, tutaongeza mawakala 4,000 wafike 10,000 ili kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema Mihayo.
Kwa upande wa mashine za ATM, alisema wigo wa upatikanaji wa huduma umekuwa maradufu, ambapo idadi ya mashine za UmojaSwitch zimeongezeka kutoka 250 mwaka 2020 hadi kufikia 281 kwa mwaka 2023 na kwamba katika kipindi hicho, benki ya TCB pia imeanza kutoa kadi za VISA.
Alisema, Umoja Switch imeingia ubia na Benki ya NMB na katika robo hii ya kwanza ya mwaka 2024, tayari kuna mashine za ATM 750 za NMB ambazo zimeunganishwa na UmojaSwitch.
“Hii inafanya jumla ya mashine za ATM za UmojaSwitch kufikia 1,031 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024,” alisema na kuongeza kuwa, TCB inajivunia kuanzisha bidhaa bora ikiwemo ile ya vikundi ambavyo vinachangishana fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii kupitia M-Koba.