KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema CCM, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutoa uongozi na kusimamia ili kuhakikisha diplomasia ya uchumi na siasa inaendelea kuiwezesha Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla, kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana ndani na nje ya nchi.
Balozi Dkt. Nchimbi alisema, mabadiliko mbalimbali ya kisera na mwelekeo, chini ya Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yameendelea kuwa sehemu ya dira ya Tanzania katika kutafuta matokeo chanya ya haraka yanayolenga kuhakikisha Tanzania inakuwa mnufaikaji sawa katika uhusiano unohusisha pande mbili, kila wakati, iwe kati ya nchi na nchi au nchi na taasisi za kimataifa.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Nchimbi alisema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Mabalozi wa Nchi za Misri na Korea Kaskazini wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, Sherif Abdelhanid Ismail na Komredi Kim Yong Su, mtawalia, pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Friedrich-Ebert-Stiftng (FES), nchini, Bi. Elisabeth Bollrich, Aprili 5, 2024, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam.
Kwa upande wake, Balozi Sherif Abdelhanid Ismail amemhakikishia Balozi Dkt. Nchimbi kuwa Nchi ya Misri, chini ya uongozi wa Rais Abd el-Fattah Saeed Hussein Khalil el-Sisi, inaichukulia Tanzania kuwa mmojawapo wa washirika wake wa karibu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ikizingatiwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na ushirikiano katika miradi mikubwa yenye athari chanya kwa uchumi wa pande zote mbili.
Naye Balozi Kim Yong Su katika mazungumzo yake na Balozi Dkt. Nchimbi alisema, Nchi ya Korea Kusini, chini ya Rais Kim Jong Un, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea (WPK), kinachoongoza nchi hiyo, ambacho ni chama rafiki na CCM.
Alisema,siku zote imekuwa tayari kudumisha na kuenzi urafiki na uhusiano wa nchi hizo mbili na vyama hivyo viwili, uliowekewa misingi imara tangu wakati wa Kiongozi wa Kwanza wa Korea Kaskazini, Komredi Kim Il Sung na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Halikadhalika, Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya FES, Bi. Elisabeth Bollrich, pamoja na masuala mengine alimwelezea Balozi Dkt. Nchimbi jinsi ambavyo FES imekuwa ikifanya kazi nchini, ambapo Katibu Mkuu huyo wa CCM alimhakikishia ushirikiano kwa masuala yenye maslahi kwa Tanzania.