Kiwango cha maambukizi ya maralia chapungua

0
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu.

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini kimepungua na kufikia asilimia 8.1 kwa mwaka 2023 kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2015.

Dkt. Jingu amesema hayo leo Machi 14, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathimini ya jitihata zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kupunguza maambukizi ya Malaria nchini.

Alisema, kupungua kwa kiwango hicho cha maambukizi ya Malaria kumetokana na jitihada za dhati za Serikali katika kuhakikisha kiwango cha Malaria nchini kinafikia sifuri kwa kuweka mikakati ya kutokomeza mazalia ya mbu sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa Vitendanishi na dawa za kutibu Malaria katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

“Serikali kupitia wizara ya afya ikishirikana na wadau wa sekta ya afya imewek dhamira ya kuhakikisha kiwango hiki cha Malaria kinapungua kabisa na kufikia ziro kwa sababu Tanzania bila Malaria inawezekana kwa kuwa na mikakati inayotekelezeka na kutoa elimu kwa jamii juu ya kudhibiti mazalia ya mbu wanaoambukiza Malaria katika makazi yao”. alisema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu ametaja mikoa ya Dar Es Salaam, Dodoma, Iringa, Songwe, Manyara, Kilimanjaro, Singida na Mwanza kuwa ni mikoa inayofanya vizuri kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria kufikia 1% na kuongeza kuwa Mikoa ya Katavi, Tabora na Kagera bado ina changamoto ya kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa huo kutokana na hali ya kimazingira ya mikoa hiyo.

“Kuna mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo jiografia ya maeneo husika kumekuwa na maeneo ambayo yana mazalia mengi ya mbu wanaoambukiza Malaria, hivyo nitoe rai kwa watanzania kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha tunadhibiti mazalia ya mbu hao”. alisema Dkt. Jingu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume alisema TAMISEMI inatekeleza na kusimamia mipango ya kupunguza ugonjwa wa Malaria kuanzia kwenye vituo vya kutolea huduma na kuzitaka Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za elimu na kinga.

“TAMISEMI tunawajibu mkubwa sana kuhakikisha vituo vyetu vya Halmashauri wametenga fedha za kutosha kwa ajili ya afua za Malaria, asilimia kubwa ya waathirika wa Malaria wako katika ngazi ya Msingi ndio maana tuna wajibu wa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama”. alisema Dkt. Mfaume.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here