Majiji manne kufungwa kamera za ‘CCTV’

0

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amekutana na Kikosi Kazi cha Miji Salama ambacho kinaratibu na kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Ufungaji wa kamera (CCTV Camera) maalumu za kuzuia uhalifu.

Kamera hizo zitafungwa katika majiji manne nchini, ambapo lengo ni kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo ujambazi, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, wizi na matukio mengine ya kiuhalifu.

Majiji yatakayofungwa kamera hizo ni Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha huku lengo likiwa kufunga kamera hizo katika mikoa yote nchini kwa siku zijazo.

“Wananchi wamekua wakikutana na kadhia hii ya uhalifu na unapotaka kudhibiti matukio ya uhalifu kwa dunia ya kisasa ni muhimu, ndio maana Serikali tumeanza jitihada za kufunga kamera, sasa mkiwa wajumbe wa kikosi kazi mfahamu mna jukumu kubwa kwa nchi kuhakikisha mradi huu unatekelezeka ili uwe na manufaa kwa nchi yetu.” alisema Waziri Masauni.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camilius Wambura amewataka wajumbe wa kikosi kazi hicho ambacho kinajumuisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanaupitia mkataba huo wa ufungaji wa kamera hizo maalumu ili lengo la mradi huo wa udhibiti wa uhalifu liweze kuleta manufaa kwa nchi.

Kikosi kazi hicho kinajumuisha wajumbe mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Serikali Mtandao na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here