Juma Duni ajitoa kugombea Uenyekiti ACT

0

HALMASHAURI Kuu ya Chama ACT Taifa iliyokutana kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo kwenye Jengo la Maalim Seif Makao Makuu ya Chama hicho, imeridhia uamuzi wa Juma Duni Haji kujitoa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa wa ACT Wazalendo.

Taarifa iliyotolewa Machi 4, 2024 ikiwa siku moja kabla ya kuanza kwa vikao vya uchaguzi Mkuu wa chama hicho, na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, ilieleza kuwa kwenye hotuba yake kwa Halmashauri Kuu, Juma Duni, Mwenyekiti wa Chama Taifa ameeleza kuwa ameshakabidhi barua yake.

“Leo tarehe 4/3/2024 mchana huu nimekabidhi rasmi barua yangu kwa Katibu wa Kamati Maalum ya Uchaguzi Taifa na kuinakilisha barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Chama na Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchaguzi Taifa – kwa taarifa na hatua zao, kuhusu kuondoa nia (kujitoa) kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa.

“Nimechukua uamuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Chama Ibara ya 11(3)(7) na Ibara ya 76(1)(p) na Ibara ya 111(3) zikisomwa pamoja, juu ya haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa Kiongozi, kazi na wajibu wa Halmashauri Kuu ya Chama kuwa ni “kujadili na kuidhinishwa na majina ya wagombea wa nafasi za Kiongozi wa Chama, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama”.

“Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwaomba viongozi wenzangu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu kuridhia kujitoa kwangu katika mchakato wa kugombea nafasi hiyo na kutopoteza muda wenu kutekeleza takwa la Katiba Ibara tajwa hapo juu,” alisema Duni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here