Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Makamu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhman Kinana, ameshauri vyama vya siasa vya upinzani hususan CHADEMA kuacha kufanya maandamano yasiyo na msingi badala yake wathamini nia njema aliyonayo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maridhiano na kuwatumikia Watanzania.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kufafanua kwa kina ubora wa sheria ya uchaguzi ambayo imepitishwa na Bunge hivi karibuni, baada ya wadau mbalimbali nchini kutoa maoni yao ambapo amesisitiza sheria hiyo ni bora kuliko iliyopo sasa.
Kinana aliyasema hayo Dar es Salaam alipozungumza na wana CCM na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo mbali ya kutumia muda mwingi kuzungumzia, maridhiano yaliyoingiwa kati ya CCM na CHADEMA pamoja vyama vingine vya upinzani, alisema kuna mambo mengi mazuri yamefanyika.
Alisema, mambo mazuri yamefanikisha kupata mwafaka ingawa CHADEMA haitaki kueleza ukweli ikiwemo serikali kukipatia chama hicho ruzuku ya Shilingi Bilioni 2.7 ambayo waliikataa kwa miaka mitatu nyuma.
Akielezea kuhusu sheria mpya, Kinana alisema pamoja na uzuri wake ikiwemo kuzingatia maoni ya wadau wakiwemo CHADEMA wenyewe, lakini bado kinasema haifai.
“Nilifikiri sheria hii mpya wangesema itatufikisha mbali zaidi, lakini wao wanasema hii haifai, basi turudi kule. Sheria ya sasa ni bora kwa muundo, kwa maudhui, kwa malengo, kwa dhamira sijui mnanielewa?. Nitumie nafasi hii kuwasihi ndugu zangu wa CHADEMA waungane na Watanzania waachane na mandamano, waangalie dhamira ya Rais.
“Hivi Rais na baraza lake la mawaziri kama wasingepeleka hii sheria mpya ya uchaguzi nani angemlazimisha? Lakini Rais busara imemuongoza akasema hapana hebu twende pamoja na mimi ndio mtetezi mkubwa wa maridhiano na ustahimilivu. Hebu tupeleke sheria mpya bungeni na kila hoja aliyopelekewa, aliyoambiwa kwamba haya ndio maoni ya wadau Rais akasema sawa, nakubali.
“Sasa niwasihi ndugu zangu Watanzania, tujipange kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, tujipange kwa uchaguzi mkuu mwaka 2025. Sheria hii ni nzuri, bora kuliko sheria yoyote iliyopo katika historia ya nchi yetu, inakidhi mahitaji na matakwa ya nchi na jumuiya ya madola, inakidhi mahitaji ya nchi za Umoja wa Afrika (AU), inakidhi vile vile mahitaji ya nchi za Kusini mwa Afrika ambao na sisi ni wanachama,” alisema.
Aliongeza kwamba, hakuna tume ya miujiza zaidi itakayokuwepo, huku akifafanua kila jambo ambalo litafanyika lazima litakuwa na kasoro moja au mbili, na kuhoji kwani CHADEMA wao hawana kasoro?.
“Wanazo, sasa nawaambia ninyi chama kikuu cha upinzani kuweni basi na ustahimilivu kidogo, uungwana na kusikiliza wenzenu na kuona nia njema iliyopo katika Chama Cha Mapinduzi, kwa na serikali yake,” alisema.
Akifafanua zaidi Kinana alisema kuwa kushinda uchaguzi kunatokana na sera, mipango ya uchaguzi na kusikiliza watu, kwani unaweza kuwa na tume nzuri ya uchaguzi na matokeo yakawa ni ya hovyo, usiyoyataka.
Alitoa mfano wa moja ya nchi jirani ambayo walipigania sana kuwa na tume huru kwa miaka 20, wakaipata, lakini wamegombea mara nne hawakupata.
“Hawakuingia madarakani, wale waliotengeneza hiyo tume hawakupata, sasa wanasema Katiba hii haina maana waifute, wale walioingizwa na katiba baadae nao wakashindwa wanasema katiba hii haina maana. Kwa hiyo aliyeshinda anasema Katiba haina maana na aliyeshindwa naye anasema Katiba haina maana.
“Sasa kushinda uchaguzi sio Katiba tu, Nigeria baada ya wanajeshi kutoka baradakani walitengeneza Katiba mpya mwaka 1969 na kwa sehemu kubwa walienda kuchukua Katiba ya Marekani, tume ya uchaguzi ya Rais inateuliwa na Rais kwa kushauriana na baraza la ushauri.
“Baraza la ushauri ni nani? Rais ndio Mwenyekiti, makamu mwenyekiti ni makamu wa rais, wajumbe wengine marais wastaafu, hapo vipi? Kuna mtu anatoka nje ya mfumo?
“Hao ndio wanateua, mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume, uchaguzi unafanyika na watu wanakubali. Hapa tunatafuta malaika wa kuja kuongoza tume, kila utakachofanya unaambiwa kinakasoro, hivi mnavyoona yote tuliyokubali wanasema hamna kitu.
“Nimesikia wanaandaa maandamano Mwanza, Mbeya na Arusha na mimi nataka niwasaidie kutangaza kama watu wengine hamjasikia. Wanakwenda kueleza haya yaliyopitishwa na CCM na Bungeni hamna kitu.
“Tume si kila kitu, Namibia kamati inatengenezwa baada ya pale anayetua Rais, kuna nchi inaitwa Mauritius na hizi nchi zote ambazo nimezitaja ni za Jumuiya ya Madola, Rais anashauriana na watu wawili tu, anashauriana na waziri mkuu na kiongozi wa upinzani bungeni hakuna mtu mwingine,” alisisitiza.
“India wana mkurugenzi na wana makamishina. Nani anateua? Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri kwisha, yaani Rais Samia akae na baraza lake la mawaziri atengeneze orodha ateue, si moto utawaka hapa? Watasema tu maigizo.
“Sasa kuna shida hapa nchini kila unalofanya halina heri ndani yake, lakini vizuri haya mambo tukayaeleza maoni mengine yakatolewa unajua siku hizi kuna watu wanapita bila kupingwa lakini ni vizuri wanaopita bila kupingwa wakapigiwa kura ya ndio au hapana Bunge likasema sawa tumekubali.
“Wanauliza kwa nini? Wanasema kuna watu wengine wanafanya ujanjaujanja wa kupita bila kupingwa, hivyo wapigiwe kura tujue kama wanakubalika Bunge limesema sawa itapigwa kura ya ndio au hapana,” alisema.
KUHUSU MARIDHIANO
Akizungumzia maridhiano ambayo yamefanyika kwa nyakati tofauti, Kinana alisema kuwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani kulikuwa na wanachama wa CHADEMA wasiopungua 400 wako mahabusu wakikabiliwa na kesi zilizotokana na sababu mbalimbali za kiuchaguzi, lakini ulitengenezwa utaratibu wa kisheria waakachiwa huru.
Kinana alisema, hakuna maridhiano bila ustahimilivu, Rais alialika taasisi za kidini na kiraia ili waelewane kujiuliza nini wanahitaji kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na taifa liwe la watu wenye mshikamano na kupendana.
Alisema, Dkt. Samia aliunda tume ya kusikiliza makundi ya Watanzania kusikiliza hoja zao ikiwemo Katiba, lakini mwishowe CHADEMA waligomea kwa sababu zao.