TET yawanoa waandishi kuhusu mtaala mpya

0
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amewasilisha mada kuhusu Mtaala ulioboreshwa kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ili kuwajengea uelewa kuhusu mtaala huo.

Dkt. Komba amefanya wasilisho hilo katika Mkutano ulioandaliwa na shirika lisilo la Kiserikali la TenMet uliofanyika katika ukumbi wa Seashells Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi kutoka TET na wadau mbalimbali wa elimu.

Katika wasilisho hilo Dkt. Komba ameeleza mtaala huu una falsafa ya kujitegemea na unamuandaa kijana mapema aweze kujiajiri au kuajiriwa kwani umejumuisha elimu ya amali (fani) na elimu ya jumla kwa pamoja.

Ameendelea kueleza kuwa, wasilisho hili kwa waandishi wa habari limekuja katika wakati muafaka kwani tayari Serikali imeanza kutekeleza Mtaala ulioboreshwa. Hivyo, waandishi wa habari ni nyenzo muhimu katika kuelimisha jamii juu ya mabadiliko ya mtaala huo.

Aidha, Dkt. Komba amewashukuru waandishi wa habari kwa kuendelea kuisaidia Serikali kutoa elimu na ufahamu juu ya umuhimu wa Mitaala iliyoboreshwa katika kuchochea maendeleo nchini kwenye ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.

Sambamba na hilo, Dkt. Komba amewatoa hofu Waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa mtaala huo, huku akisisitiza Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha wanafunzi wananufaika na mtaala huo ikiwemo upatikanaji wa vitabu vya kiada.

Nae, Mkurugenzi wa Mafunzo na Mitaala Dkt. Fika Mwakabungu alisema, tayari TET imeshatoa mafunzo kwa Maafisa Elimu Mkoa, Wilaya, kata, wathibiti ubora wa elimu na baadhi ya walimu kutoka shule za Serikali na zisizo za Serikali, jambo linalochochea kwa kasi utekelezaji wa mtaala huu ulioboreshwa nchini.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu na Ukuzaji Mitaala TET Dkt. Godson Lema amesema katika utekelezaji wa Mitaala hii tayari Serikali imeidhinisha shule 96 zilizokidhi vigezo zitakazoanza kutekeleza mkondo wa Amali (fani) kwa elimu ya sekondari huku ikiendelea kuzijengea uwezo shule nyingine ili kufikia vigezo hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here