Nchi jirani zavutiwa na mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja

0
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Erasto Mulokozi akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusiana na mafanikio ya PBPA.

Na Iddy Mkwama

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja ( Petroleum Bulk Procument Agency – PBPA), Erasto Mulokozi amesema, wanapokea wawakilishi wa nchi mbalimbali wanaokuja kujifunza kuhusu Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procument System – BPS).

Mulokozi alisema hayo Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa lengo la kuelezea majukumu na mafanikio ya PBPA na ufanisi wa mfumo wa BPS.

Alisema, miongoni mwa nchi ambazo zimekuja kujifunza kuhusu mfumo huo na wengine wapo mbioni kuja nchini ni DRC, Uganda, Rwanda, Namibia na Msumbiji.

Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Sabato Kosuri, akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi cha Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency – PBPA) na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

“Wenzetu wa nchi jirani wanakuja kujifunza kuhusu mfumo huu ambao una mafanikio makubwa kwa nchi yetu, Msumbiji wao walikuwa nao, lakini huu wetu umeboreshwa zaidi, hivyo wanakuja kujifunza,” alisema Mulokozi.

Alisema, tangu Serikali ilipoanzisha wakala wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, yamepatikana mafanikio mengi ikiwemo uhakika wa upatikanaji wa mafuta ambayo yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaotakiwa wakati wote.

“Wakala wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja ulianzishwa kwa amri ya Serikali (establishment Order, 2015) chini ya mwongozo wa sheria ya wakala wa Serikali (The executive Agencies Act – Cap 245) kwa lengo la kuratibu na kusimamia mfumo wa BPS, yamepatikana manufaa ya kiuchumi na nchi ina uhakika wa upatikanaji wa mafuta,” alisema Mulokozi.

Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari katika mkutano na PBPA.

Alisema, matumizi ya mfumo huo yanasaidia kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni 500 kila mwaka, sambamba na kupata unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta “Mfumo huu umechangia kupungua kwa bei ya mafuta kutokana na uagizaji wenye ufanisi ikiwemo kuongezeka kwa mapato ya kikodi yatokanayo na bidhaa ya mafuta.”

Aidha, alisema mfumo wa BPS umewezesha kupunguza vitendo vya ukwepaji kodi kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya waagizaji wa mafuta “Mfumo umewezesha kudhibiti udanganyifu katika gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uletaji wa mafuta nchini,”

Alisema, mfumo huo pia umesaidia kupunguza msongamano wa meli bandarini; awali kila kampuni ilikuwa inaagiza mafuta yake, hivyo unakuta mzigo ni mdogo ila meli zipo nyingi, kwahiyo inachukua muda mrefu kushusha mzigo.

Baadhi ya Wahariri wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi huyo wakati akijibu maswali na baadaye kufunga kikao hicho kwa kutoa neno la Shukurani kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Msajili wa Hazina na Wahariri hao.

“Hivi sasa tunaagiza mzigo mkubwa kwa pamoja na unashushwa kwa wakati, hiyo mbali na kupunguza gharama, lakini inaokoa zaidi ya Shilingi Bilioni 425 ambazo zilikuwa zinatumika kama gharama za kulipigia wakati unasubiri kushusha mzigo bandarini,” alisema.

Mulokozi alisema, katika kuboresha zaidi utendaji wa PBPA, Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka mitatu wamedhamiria kujenga miundombinu ya kupokea meli za mafuta ili kupunguza siku za kukaa bandarini kwa ajili ya kusubiri kushusha mzigo.

Mbali na hilo, alisema Serikali imefanya imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa ruzuku kwenye gharama ya mafuta kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai, 2022 hadi Disemba, 2022 kupunguza bei ya mafuta kwa wananchi na kuwa bei stahimilivu kwa mlaji wa mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here