‘Ni muhimu Taifa kuwa na watu mahiri na waadilifu’

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameainisha changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele ikiwemo kufungamanisha ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji.

Rais Samia alisema hayo kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara sanjari na Mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi wa Mchakato wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Rais Samia alifanya uzinduzi huo wakati wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Aidha, Rais Samia ametaka sekta mbalimbali za uzalishaji ziimarishwe zaidi ikiwemo kilimo ambayo inakua kwa asilimia 4 tu kwa sasa tofauti na inavyotakiwa.

Pia, alisisitiza kuimarishwa kwa ushiriki wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi ili kufanya wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja kuwekeza na kufanya biashara nchini.

Rais Samia alisema, dira hiyo mpya itatakiwa kuzingatia kigezo cha kuongeza pato la kila mwananchi kufikia dola za Kimarekani 3,000 kwa mwaka ambacho hakikufikiwa katika dira ya mwaka 2000-2025.

Viongozi, pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye Maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara pamoja na uzinduzi wa Mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma

Alisema, kushindwa huko kulisababishwa na ukuaji wa uchumi kutojielekeza kwenye sekta zinazogusa maisha ya watu wengi, hivyo umasikini vijijini haujapungua kwa kasi iliyotarajiwa.

Kuhusu suala la Maadili ya Taifa (ethos), Rais Samia amesema ni muhimu taifa kuwa na watu mahiri, makini na waadilifu ili kupata jamii inayochukia rushwa kila mahali, inayojituma na kufanya kazi bila kusukumwa na inayopinga na kulaani ukwepaji kodi.

Vile vile, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi (Diaspora) kushiriki kutoa maoni katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo kupitia njia za kisasa zitakazoainishwa na Tume ya Mipango.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri wakati akielezea majukumu ya Kituo wakati wa Maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here