Watanzania watakiwa kutunza rasilimali za misitu

0

Na Jumbe Abdallah

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watunze rasilimali za misitu kwa kuwa zinafaida kubwa kwa Dunia, Taifa na mwananchi mmoja mmoja.

Alisema, katika vipindi tofauti Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu nchini, hivyo kila mmoja ahakikishe anazingatia suala hilo.

Majaliwa alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kagunga Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi baada ya kukabidhi hundi mbili zenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.27. Fedha hizo zilizotolewa na taasisi ya CARBON TANZANIA kwa wananchi wa vijiji vinane na Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika zimetokana na mauzo ya hewa ya ukaa awamu ya sita.

“Fedha hizi mmezipata kutokana na tabia yenu nzuri ya utunzaji wa misitu, endeleeni kuitunza misitu hii ili tupate mvua za kutosha. Pia, tumieni mvua hizi zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao mbalimbali.”

Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini waendelee kuweka mikakati ya kuwaelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira. “Kila mtumishi wa umma kwenye eneo lake ahakikishe moja ya agenda iwe uhifadhi wa mazingira.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka halmashauri zote zenye miradi ya hewa ukaa zifuatilie mikataba inayosainiwa baina ya makampuni na vijiji kwa ajili ya mauzo ya hewa hiyo. “Mikataba hii ni lazima tuijue, wanasheria wetu lazima muifuatilie.”

Waziri Mkuu amewataka wana-Vijiji watumie fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya hewa ya ukaa kwa maslahi ya wananchi wote. “Wakurugenzi fuatilieni kama mipango ya wanavijiji ina maslahi kwa wananchi wote, jengeni miundombinu ya umma, posho isichukue nafasi kubwa.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here