KAMPALA, Uganda
JESHI la Ulinzi la Uganda (UPDF) limesema litatuma mamia ya askari wake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na kikosi cha kieneo kinachopambana na magenge ya waasi na wabeba silaha Mashariki mwa DRC.
Akinukuliwa na Pars Today Msemaji wa Jeshi la Uganda Felix Kulayigye alisema, nchi hiyo itatuma wanajeshi 1,000 nchini DRC mwishoni mwa mwezi huu kwenda kuwa sehemu ya kikosi cha pamoja cha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Haya yanajiri siku chache baada ya kundi la pili la wanajeshi wa Kenya kuwasili katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lililoathiriwa na machafuko na hujuma za waasi.
Wanajeshi hao 900 wa Kenya wametumwa Kongo katika fremu ya kikosi cha kudumisha amani cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Viongozi wa nchi za jumuiya ya EAC Juni mwaka huu walikubaliana kutuma kikosi cha kikanda Mashariki mwa Kongo DR kwenda kukabiliana na waasi wa M23 na magenge mengine ya wabeba silaha.
Wanajeshi wa Kenya waliotumwa DRC
Wanajeshi wa Kenya waliwasili katika mji wa Goma siku chache zilizopita, wakati kundi la waasi la M23 likiwa limeingia katika jimbo la Kivu Kaskazini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuteka maeneo mengi na hivyo kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo la Maziwa Makuu.
Ikumbukwe kuwa, Septemba mwaka huu, Uganda iliipa Kongo DR Dola Milioni 65, kama sehemu ya kwanza ya fidia ya Dola Milioni 325, kutokana na hasara ambazo wanajeshi wa Uganda waliisababishia nchi hiyo miaka ya 90.