Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Idara ya habari na Mawasiliano wa timu ya Polisi Tanzania Frank Lukwaro amesema, kikosi chao kimejipanga kuibuka na ushindi katika mchezo wake wa ligi kuu dhidi ya Dodoma jiji unaotarajiwa kufanyika Jumanne hii katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Lukwaro alisema, kikosi chao kimekuwa kikiendelea kuimarika kadri siku zinavyozidi kwenda kutokana na kuweka mikakati madhubuti ya ushirikiano wa pamoja baina ya Uongozi, Benchi la ufundi na Wachezaji.
“Tumezungumza na Wachezaji wetu watupe furaha katika mchezo huu hasa ukizingatia kuwa hatupo katika sehemu salama katika msimamo wa ligi hii inayoendelea na ndio maana tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujinasua katika nafasi za chini na hilo litafanikiwa,” alisema Lukwaro.
Aidha, alisema suala la kumpata Kocha mkuu baada ya kumtupia virago Joslin Sharif linaendelea kufanyiwa kazi na uongozi na taarifa itatolewa hivi karibuni kwa kuwa lipo katika hatua za mwisho.
Alisema, wana idadi kubwa ya makocha waliopo ndani ya Jeshi la Polisi wenye vigezo na hata kutoka nje ya Polisi pia wapo ambao wamekuwa katika mipango yao hivyo mashabiki wao wasiwe na wasiwasi.