Putin yupo tayari kupunguza mvutano na Ukraine

0

MOSCOW, Russia

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amesema, Rais Vladimir Putin yuko tayari kufanya mazungumzo na nchi za Magharibi kuhusu Ukraine.

Russia imekuwa ikiendesha operesheni ya kijeshi nchini Ukraine tangu Februari huku nchi za Magharibi zikiipa nchi hiyo idadi kubwa ya silaha.

“Tuko tayari kuzungumza na nchi za Magharibi kuhusu kupunguza mvutano,” alisema Lavrov na kuongeza kuwa, “matarajio ya mazungumzo, hata hivyo, yatatimia ikiwa tu kuna mapendekezo yenye kuzingatia uhalisia wa mambo kulingana na muelekeo sawa.”

Mwanadiplomasia huyo Mkuu alibainisha kuwa, Putin amekuwa akisema mara kwa mara kwamba, Russia haijawahi kukataa pendekezo la mazungumzo, akisema “Ukraine ndiyo iliyokataa mazungumzo chini ya maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa wafadhili wake wa Magharibi.”

Aidha, Lavrov amelinganisha hali ya Ukraine na mgogoro wa Cuba wa 1962, wakati Shirikisho la Sovieti na Marekani zilikaribia kuingia katika vita vya nyuklia.

Wakati huo, Rais wa Marekani John F. Kennedy aligundua kuwa kiongozi wa Shirikisho la Sovieti Nikita Khrushchev alikuwa amepeleka makombora ya nyuklia nchini Cuba.

Ili kutatua mgogoro huo, Kennedy alikubali kwa siri kuondoa makombora yote ya Marekani kutoka Uturuki ili kubadilishana na Khrushchev kuondoa makombora ya nyuklia kutoka Cuba.

Lavrov alisema, kuna kushabihiana kati ya hali ilivyo sasa nchini Ukraine na mzozo wa Cuba, haswa kwa sababu Russia sasa inatishiwa na silaha za Magharibi huko Ukraine.

“Hali hii inasumbua sana. Tofauti ni kwamba, mwaka 1962, Khrushchev na Kennedy walipata nguvu ya kuonyesha uwajibikaji na busara, lakini sasa, hatuoni utayari kama huo kwa upande wa Washington na waitifakie wake.”

Russia imeishutumu Marekani na washirika wake wa Magharibi kwa kuipa Ukraine idadi kubwa ya silaha, na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa jamhuri hiyo ya zamani ya Shirikisho la Sovieti.

Aidha, Russia inasema madola ya Magharibi yanaiunga mkono Ukraine ili kurefusha mapigano kwa lengo la kuidhoofisha na kuichosha Russia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here